Na Mario Mgimba Njombe
Jeshi la polisi mkoani Njombe limekamata mali mbalimbali za wizi katika maeneo tofauti huku likikamata pia vitabu vya dini na vifaa vingine ambavyo ni mali ya kanisa la Roman Katholiki mjini Njombe .
Akizungumza na Vyombo vya habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Hamis Issa wakati akitoa taarifa ya mafanikio ya Jeshi la polisi katika kipindi cha mwezi Novemba hadi sasa amevitaja vitu vilivyoibwa na kukamatwa kuwa ni pamoja na TV,Pikipiki,Magodoro,Mabero ya mitumba,kichwa cha cherehani,simu pamoja na mali nyingine.
Kamanda Issa amesema watuhumiwa hao wamekamatwa na vifaa hivyo wakati wa doria zilizokuwa zikifanywa na Askari katika maeneo mbalimbali.
Aidha Kamanda Issa pia ameonya watu watakaojaribu kuacha kufanya shughuli halali na badala yake kujiingiza kwenye wizi kwani hawatoachwa salama kwa kuwa jeshi hilo linafanyakazi wakati wote.
Baadhi ya wakazi wa Njombe akiwemo Ibrahim Mvelu na Abel Torino Kipuga wanasema vitendo vya wizi vimekuwa vikiwarudisha nyuma kimaendeleo wananchi jambo linalopaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria pindi wahalifu wanapokamatwa.
Matukio ya kihalifu yamekuwa mwiba kwa maendeleo ya wananchi hapa mkoani Njombe kwani yamekuwa yakisababisha raia kushindwa kufanya maendeleo wakihofia kuibiwa mali zao pindi wanapotaka kununua jambo ambalo halipaswi kufumbiwa macho katika Taifa huru la Tanzania.
Post A Comment: