Hospitali ya Taifa Muhimbili imepokea msaada wa vifaa tiba mbalimbali vyenye thamani ya TZS. 50 Mil kutoka Faidika Microfance Bank (FMB) na Letshego Bank ambavyo vitatumika katika wodi ya watoto kwa lengo la kuendelea kuboresha hali utoaji huduma.

Msaada ni pamoja na mashine ya kupima uzito, mashine ya uangalizi wa mapigo ya moyo ya mgonjwa, kupima joto la mwili na kiasi cha oxygen mwilini .

Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam, Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Rashid Mfaume amesema Muhimbili inafanya kazi kubwa ya kutoa huduma hivyo msaada huu ni muhimu katika kuendelea kuboresha huduma za afya hivyo amewataka wadau wengine kuendelea kuunga mkono juhudi hizo.

“Hili ni jambo kubwa sana hivyo tunaomba wadau wengine wanaoguswa kujitoa na kusaidia kama hawa walivyoguswa na kuamua kutusapoti , vilevile hapa sio kama tumekuja kupokea msaada tu bali tunatengeneza undungu ambao utaleta manufaa kwa pande zote mbili,” amesema Mganga Mkuu wa Mkoa. Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amewashukuru Faidika Bank pamoja na Letshego Bank kwa msaada huo na kusisitiza kuwa ni jambo kubwa kwa Muhimbili kuwa na vifaa vya kisasa ambavyo vitasaidia utoaji huduma katika wodi ya watoto.

“Sisi kama madaktari monitor hizi zitaenda kusaidia kujua hali ya mgonjwa na maendeleo yake, pia kujua kiwago cha joto kwa mgonjwa na kujua mapigo ya moyo, leo tuna watoto 318 kati ya hao takribani 215 ni wagonjwa wa saratani za watoto, lakini pia wapo wenye matatizo ya moyo, walioungua na wenye magonjwa ya kuzaliwa hivyo ni muhimu kuwa na vifaa vya kisasa” amesema Prof. Janabi

“Muhimbili ni hospitali kubwa inavitanda 1500, tuna hospitali nyingine Mloganzila ambayo inavitanda 608 , MNH tunaona wagonjwa 2000 kila siku wanaokuja kwenye kliniki zetu mbalimbali kupata matibabu na hawa ni mbali ya wale takribani 700 tunaowaona Mloganzila ambapo kuna vitengo vyetu vikubwa vitatu ikiwemo kitengo cha moyo, kisukari na kitengo cha mishipa ya fahamu pamoja na huduma nyingine mbalimbali,” amefafanua Prof. Janabi

Kwa upande wake, Bw. Philip Odera kutoka Letshego Bank amesema wao kama wadau ni jukumu lao kusaidia jamii ndiomaana wamefika Muhimbili ili kutoa msaada wa vifaa tiba ambavyo wanaamini vitaendelea kuboresha huduma.

“Tumetoka nchi mbalimbali wapo waliotoka Botswana, Nigeria, Afrika Kusini , Marekani lengo ni kushirikiana ili kusaidia jamii na hili ni muhimu kwetu,’’ amesema Bw. Odera
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: