Kamati ya siasa ya chama cha mapinduzi 'CCM' mkoa wa Tanga ikiongozwa na mwenyekiti wake Rajabu Abdurahman imekataa taarifa ya mganga mkuu wa wilaya ya Pangani Maulid Majala kuhusiana na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Ushongo pamoja na nyumba ya Muuguzi katika kata ya Mwera ambapo licha ya kuongezewa fedha na serikali shilingi Million 150 kwaajili ya kuukamilisha tangu February mwaka huu lakini mpaka sasa bado una sua sua.
Hayo yamejiri wakati kamati hiyo ilipofanya ziara ya kutembelea Zahanati hiyo iliyojengwa kwa nguvu za wananchi na baadaye serikali ikaongeza kiashi cha shilingi Million 150 kwaajili ya kumalizia na kuanza kutoa huduma kwa wananchi lakini taarifa iliyotolewa inakinzana na uhalisia wa maendeleo ya mradi yaliyopo kwa sasa.
Aidha umaliziaji wa Zahanati hiyo unaenda sambamba na ujenzi wa nyumba ya wahudumu wa afya ambao bado haujaanza kutekelezwa hatua ambayo imemfanya mbunge wa jimbo hilo Jumaa Aweso kuongeza kiasi cha Shilingi Million tano kwaajili ya kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Akitoa taarifa za utekelezaji wa mradi huo mganga mkuu wa wilaya ya Pangani Maulid Majala alisema kuwa kumekuwa na changamoto ya kumalizika kwa ujenzi huo kutokana na kuchelewa kwa muda wa kuomba kubadilisha matumizi ya fedha hadi kufikia sasa akiieleza kamati hiyo kuwa fedha zilizopo zilishahamishwa kutoka kwenye akaunti ya Zahanati hadi kwenye mradi jambo ambalo limeonekana sio la kweli.
"Kumekuwa na changamoto ya kuchelewa kuanza kwa mradi huu kutokana na muda wa kuomba kubadilishia matumizi ya fedha na vifungu vya matumizi kulikopelekea fedha hizi kuvuka mwaka, fedha za mradi huu zilishahamishwa kutoka kwenye akaunti ya Zahanati kwaajili ya utekelezaji wa mradi" alisema Majala.
Awali akizungumza mweyekiti ya kamati ya huduma za jamii wa wilaya hiyo ambaye pia ni diwani Akida Boramimi alisema kuwa kamati yake ilifanya ziara ya kutemblea maendeleo ya mradi huo na kutoa maagizo ambayo ni pamoja na kuhamisha fedha kwenda kwenye mradi , kusambaza vifaa vya ujenzi lakini jambo hilo halikutekelezeka kwa wakati.
"Hatua ya utekelezaji wa ujenzi wa nyumba ya Mganga mimi nilifanikiwa kufika hapa kwaajili kukagua baada ya kuona fedha hizi zimevuka mwaka, tulitoa maagizo ya kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti ya mkurugenzi kwenda kwenye akaunti ya mradi, tuliagiza wazabuni watafutwe na shughuli za kusambaza vifaa vya ujenzi na shughuli nyingine zianze lakini jambo hilo mpaka sasa halijatekelezeka" alisema Boramimi.
Akizungumza na wananchi wa kata ya Mwera katika mkutano wa hazara Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi mkoa wa Tanga Rajabu Abdurahman amemtaka mkurugenzi wa halmashauri pamoja na mganga mkuu wa wilaya hiyo kujitafakari kufwatia kusua sua kwa mradi huo na kusema kuwa hwatokubali watendaji ambao wamekuwa hawawajibiki ipasavyo katika majukumu waliyopewa.
"Zahanati ya Ushongo wananchi waliijenga kwa fedha zao wenyewe walizochanga kupitia serikali ya kijiji, ili weweze kupata huduma za afya karibu, zahanati ile haijakamilika, mbunge kaenda kutafuta fedha million 150 huu ndio mchakato wa kimaendeleo tunaotaka lakini halmashauri wamezembea toka mwezi wa pili mpaka leo sisi kama chama cha mapinduzi hatuwezi kukubali, "
"Tumetoa kauli mkurugenzi ajitafakari na mganga wa wilaya ajitafakari , na hizi ni salamu zote kwa mkoa wa Tanga , miradi yote ambayo serikali inaleta fedha kwa wakati tunahitaji tuone maendeleo kwa wakati wala hatuhitaji maneno mengine" alisema Adurahman.
Mbunge wa jimbo la Pangani ambaye pia ni waziri wa maji Jumaa Aweso alisema kuwa kuzorota kwa miradi mbalimbali ya serikali katika wilaya hiyo imekuwa ni kasumba ya muda mrefu sasa ifike mahali wahusika wanaosimamia miradi hiyo wachukuliwe hatua pale wanaposhindwa kuwajibika ipasavyo.
"Ukiangalia mradi huu wananchi wamejenga kwa fedha zao, utekelezaji wa mradi unategemena na fedha , tumeomba fedha zimekuja million 150 sasa kama fedha zipo lakini zinavuka mwaka bado tunababaishana hii sio sawa hapa tunazungumza uhai na maisha ya watu wetu viongozi mpo mkurugenzi na mkuu wa wilaya haiwezekani huu ni udanganyifu haya mengine ni ya kuchukulia hatua ili tuweze kwenda, tukioneana haya hakuna mambo yataweza kwenda katika wilaya yetu ya Pangani"
alisema Aweso
Hata hiyo mradi huo wa Zahanati pamoja na nyumba ya Muuguzi imepangwa kukamilika ndani ya miezi mitatu ili hatimaye wananchi wa kata ya Mwera waanze kupata huduma za afya badala ya kwenda mbali kama ilivyo kwa sasa.
Mbunge wa jimbo la Pangani na waziri wa maji Jumaa Aweso akizungumza na wananchi wa kata ya Mwera katika mkutano wa hazara wa chama cha mapinduzi 'CCM' mkoa wa Tanga.
Post A Comment: