Katibu tawala wilaya ya Korogwe Rachel Mhando akifungua semina kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Tanga kuhusu mradi wa Shule Bora unaofadhiliwa na Serikali ya Uingereza , ambapo unatekelezwa katika mikoa 9 hapa nchini.
Na Denis Chambi , Tanga.
Jumla ya mikoa tisa ya Tanzania bara inatarajiwa kunufuika na mradi wa shule bora wenye lengo la kuboresha na kuinua kiwango cha elimu kwa wanafunzikuanzia ngazi ya awali mpaka darasa la saba utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka 6 .
Mradi huo ambao unatekelezwa na serikali ya Tanzania ukifadhiliwa na serikali ya uingereza umelenga pia kuboresha ufundishaji kwa walimu, kuboresha elimu jumuishi kwa makundi ya watoto wenye mahitaji maalum , kuboresha ujifunzaji kwa wanafunzi pamoja na kuboresha mfumo wa usimamiaji wa sekta ya elimu katika kuhakikisha kila kiongozi anawajibika ipasavyo kwa nafasi yake ili kufikia adhima iliyokusudiwa.
Aidha mradi huo umekuja kwa malengo mahususi ya kuangazia na kuondoa kabisa changamoto za watoto wengi kushindwa kusoma , kuandika na kuhesabu vizuri, tatizo la utoro mashuleni , kupambana na mimba za za utotoni kuwapa fursa watoto wenye mahitaji maalumu katika kuendelea na elimu ya sekondari ambapo wengi wao wamekuwa wakishindwa kuendelea kutokana na vikwazo mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari walioshiriki semina ya kuutambulisha mradi huo mratibu Thomas Aikaruwa amesema kuwa licha ya mradi huo kutekelezwa kwa kipindi cha miaka 6 lakini pia wanakusudia kuongeza muda wa miaka mitatu ambapo itatokana na matokeo yatakayopatikana kwa kipindi chote cha utekelezaji.
Alisema kwa kutambua mchango wa waandishi wa habari ambao pia wadau muhimu katika mradi huo na maendeleo ya sekta ya elimu kwa ujumla hapa nchini wanatarajia kuifikia jamii katika kuwaelimisha , kuhamasisha kwa kupitia vyombo vya habari matarajio yakiwa ni kuweza kuleta matokeo chanya ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanapatikana.
"Matarajio yetu makubwa tuliyonayo ni kuona elimu ya msingi inaboreka na tumeshaanza kuona dalili njema za kuboresha elimu hii kwahiyo tunategemea baada ya miaka hii ya utekelezaji wa mradi tuone hali tofauti kwenye mikoa hii 9 katika sekta ya elimu tuone mahudhurio ya watoto mashuleni yanaboreka , kujua kusoma na kuandika vizuri kabisa , tuone watoto wa kike wakiwa wanapata fursa sawa sawa na watoto wa kiume na watoto wenye mahitaji maalumu wanaendeleea na elimu ya sekondari." alisema Aikaruwa.
"Waandishi wa habari ni wadau muhimu sana tuliona ipo haja ya kuita waandishi wa habari tuje tufanye nao kazi hii katika kuelimishana kuhusiana na mradi huu , tunaomba waandishi wa habari watusaidie kuieleza jamii mambo ambayo serikali imetoa nguvu kubwa katika kuboresha elimu hii" aliongeza.
Awali akifungua semina hiyo kwa waandishi wa habari katibu tawala wilaya ya Korogwe Rahel Mhando amewaasa wanahabari kutumia kalamu zao vizuri katika kuelimisha jamii juu ya mradi huo wakizingatia taratibu, kanuni sheria zinazowaongoza katika taaluma yao
"Ili kuweza kuboresha na kufanikisha malengo mahususi mradi unaamini mawasiliano kupitia vyombo vya habari ni nyenzo muhimu sana ili kuifikia jamii kubwa zaidi , jukumu la kuhakikisha taarifa zote za shughuli za mradi na maendeleo yake katika mkoa wetu wa Tanga ni la kwetu sote hivyo kila mmoja wetu anatakiwa kutekeleza jukumu hilo kwa uhakika , weledi na kwa uadilifu kwa lengo la kuhakikisha watoto wetu wanapata elimu iliyobora "alisema Mhando.
Afisa elimu mkoa wa Tanga Newaho Mkisi amebainisha kuwa kwa sasa bado ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ni wa wastani lakini ujio wa mradi huo utakwenda kusaidia na kuongeza kiwango cha ufaulu hatua ambayo itakwenda kuuwezesha mkoa kupata fedha zaidi zinazotolewa na serikali kupitia mradi wa lipa kwa matokeo 'Ep forR, ambazo hutolewa kulingana na vigezo na masharti yaliyowekwa na seikali zikiwa na lengo la kuendelea kuweka mazingira rafiki katika sekta ya elimu hapa nchini.
"Mkoa wetu umeongeza ufaulu ukiangalia kwa ufaulu wa mwaka jana ukilinganisha na mwaka huu japo sio kwa wastani mkubwa kwenye mradi wa EpforR tulikuwa tunashindwa kupata fedha nyingi kwa sababu tulikuwa tunashindwa kufikia vile vigezo vilivyowekwa ikiwemo ufaulu ili tuweze kupata ufaulu mzuri lazima fufanye kazi kwa kushirikiana tukikidhi hivyo vigezo tunapata fedha zaidi abazo zitasaidia katika maswala ya elimu" alisema Mkisi.
Mikoa itakayonufaika na mradi huo wa shule bora kwa kipindi chote cha utekelezaji kwa miaka 6 ni Tanga, Dodoma , Pwani , Katavi, Kigoma , Mara, Rukwa , Singida na Simiyu
Mratibu wa mradi wa Shule Bora Thomas Aikaruwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya semina iliyofanyika wilayani Korogwe December 6,2022.
Post A Comment: