Na John Walter-Manyara

Leo Desemba 9, Tanzania inakumbuka ilivyopata Uhuru wake miaka 60 iliyopita wakati huo ikifahamika kama Tanganyika kabla ya kuungana na Zanzibar na kuwa nchi Moja.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwaka 2022, Idadi ya Watanzania inatajwa kuwa na wakazi Milioni 61 wastani wa ongezeko la watu Milioni Moja kila mwaka kuanzia kupatikana kwa Uhuru mwaka 1961.

Bi. Mansueta Sanka aliewahi kufanya kazi ndani ya Chama Cha TANU na nafasi mbalimbali serikalini alishuhudia sherehe za Uhuru mwaka 1961 akiwa kidato cha Kwanza, anasema Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa na hekima kubwa ndo maana nchi ilifanikiwa kupata Uhuru mapema.

Sanka akizungumza katika mdahalo maalum wa kumbukizi ya Uhuru ambapo kwa mwaka huu ni miaka 61,  anaeleza kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa muumini wa Siasa safi na hakuvibagua vyama vingine.

Amesema baada ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania bara) Nyerere alianzisha Ujamaa na kujitegemea mfumo uliowaweka watu karibu, hali iliyowezesha huduma za kijamii kupatikana kiurahisi kwa watu wote.

Anakumbuka kulikuwa na vyama vingine tofauti na TANU na ASP lakini vilipotea kutokana na nguvu ya vyama hivyo viwili.

Mzee Jasson Begashe aliekuwepo kabla ya Uhuru na baada ya Uhuru anasema Kuna mabadiliko makubwa kwa sasa ndani ya nchi kwenye kila sekta.

Mbunge wa zamani wa jimbo la Babati Vijijini (CCM) Jitu Vrajlal Son amesema miundombinu ya barabara imeboreshwa kwa kiwango kikubwa tofauti na kabla ya Uhuru.

Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Babati Anna Fissoo amesema kwa sasa tunasheherekea matunda mazuri yaliyopandwa na waasisi wa Taifa.

"Kwenye elimu nchi imepiga hatua Kubwa ambapo serikali imejenga shule kila Kijiji na kila kata huku wanafunzi wakisoma bila malipo kuanzia Elimu ya msingi hadi kidato cha sita" alisema Fissoo.

Tanzania bara inatimiza miaka 61 ya uhuru huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Samia Suluhu Hassan akielekeza fedha zilizotakiwa zitumike kwenye maadhimisho ya siku hii zitumike kuendeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo kuboresha shule za misingi katika maeneo mbalimbali ya Tanzania kwa lengo la kuhakikisha changamoto ya upungufu wa madarasa inamalizika hapa nchini.

Share To:

Post A Comment: