Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh.Anthony Mavunde amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia madarasa ya uanzishwaji wa Shule mbili mpya za Msingi na Sekondari katika kata ya Mpunguzi,Jijini Dodoma.


Mavunde ameyasema hayo jana Mpunguzi wakati wa ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Shule mpya ya Msingi Mlangwa B na Sekondari mpya ya Nkulabi.

“Mwezi Agosti,2022 wakati Mh Rais amesimama hapa Mpunguzi tulimuomba madarasa kwa ajili ya uanzishwaji wa Shule mpya za Msingi Mlangwa B na Sekondari Nkulabi ili kuwapunguzia mwendo watoto hawa wa Shule ambao wanatembea kilomita 9 kufuata shule.

Tunamshukuru Mh Rais kwa kulipokea ombi letu na sasa utekelezaji umeanza rasmi.

Niwashukuru wananchi wote kwa kujitolea nguvu kazi na kuufikidha huu mradi mpaka hapa ulipofika.

Rai yangu kwa wataalamu wetu ni kuhakikisha mnasimamia vizuri ujenzi wa shule hizi kwa ubora wa hali ya juu na mradi ukamilike kwa wakati ili mapena tarehe 9.01.2023 watoto waanze kuyatumia hayo majengo”Alisema Mavunde

Akitoa maelezo ya awali Diwani wa Kata ya Mpunguzi Mh. Innocent Nyambuya amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapunguzia mwendo watoto wa Mpunguzi kupitia ujenzi wa shule hizo na pia ametoa shukrani kwa Mbunge Mavunde kwa kuwa nao bega kwa bega wakati wote wa utekelezaji wa miradi hii sambamba na misaada mikubwa ya vifaa vya ujenzi alivyotoa kuunga mkono jitihada hizi za serikali.







Share To:

Post A Comment: