Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Taifa, Mohamed Ali Mohamed maarufu kama Kawaida ameitaka Serikali ya mkoa wa Dar es Salaam kuangalia upya faini za waendesha bodaboda.
Kawaida amebainisha hayo leo Desemba 23, 2022 wakati wa hafla ya mapokezi yake katika mkoa wa Dar es Salaam ikiwa ni siku chache tangu amechaguliwa kuongoza jumuiya hiyo ya CCM.
Amesema faini ya Sh70,000 wanayotozwa bodaboda barabarani ni kubwa, hivyo serikali iliangalie jambo hilo ili vijana hao waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.
"Nimepokea malalamiko ya vijana wa Dar es Salaam, nimeona niyafikishe kwa Serikali ya mkoa. Watu wa bodaboda bado hawajaelewa vizuri.
"Kwa kweli faini ya Sh70,000 ni nyingi sana, ninaomba serikali mliangalie hili," amesema Kawaida akielekeza kilio hicho cha waendesha bodaboda kwa mkuu wa wilaya ya Ubungo ambaye alikuwa akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla.
Kawaida amewataka kwenda kutoa elimu zaidi kwa vijana hao kwa sababu ameona kwamba hawana uelewa wa kutosha juu ya hatua zinazochukuliwa na serikali ya mkoa.
Wakati huohuo, Kawaida amesema wanakwenda kuendeleza miradi mbalimbali ya jumuiya na kwamba vijana wengi watanufaika na miradi hiyo huku akiwahimiza kuilinda.
"Mradi uliopo ndani ya kata yako, wilaya yako, mkoa wako, ni jukumu lako kuulinda. Naomba sana tushirikiane katika kuijenga jumuiya yetu na chama chetu," amesema Kawaida
Post A Comment: