Angela Msimbira ARUSHA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Angellah Kairuki amewataka Viongozi wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha wanasimamia kwa ufanisi utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa elimu ya Awali na Msingi ili kufikia malengo ya serikali ya kutatua changamoto za elimu nchini.
Ameyasema hayo leo tarehe 13 Disemba, 2022 wakati akifunga kikao kazi cha kuwajengea uwezo Makatibu Tawala wa Mkoa, Maafisa Elimu wa Mkoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu utekelezaji wa wa Mradi wa Boost, kilichofanyika Jijini Arusha.
Waziri Kairuki amewataka kuzingatia sheria, kanuni na miongozo katika utekelezaji wa mradi ili thamani ya fedha iliyotolewa iendane na majengo yatakayojengwa na amwaagiza kuepuka hoja za ukaguzi
Vilevile, Waziri Kairuki ameonya tabia ya baadhi ya Halmashauri kubadilisha maeneo ya ujenzi au kukarabatiwa kwa shule kwa kuwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI ilishafanya tathmini na kugundua kuwa zipo shule ambazo zinahitaji ukarabati wa miundombinu kutokana na uchakavu hivyo maamuzi ya Serikali yamezingatia viashiria vya msongamano wa wanafunzi, vijiji vyenye ukosefu wa shule za msingi na maeneo ambayo wanafunzi wanatembea umbali mrefu.
Waziri Kairuki amesema katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali itatoa shilingi bilioni 240 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi,hivyo amewaagiza kusimamia ujenzi huo ili ukamilike kwa wakati kwa kuzingatia miongozo na wajiepushe na migogoro ambayo huchangia kuchelewesha utekelezaji wa miradi
Aidha amewataka viongozi hao kuhakikisha wanaimarisha ushirikiano na Taasisi na Idara mbalimbali katika utekelezaji wa baadhi ya afua za Mradi wa BOOST ili kufanikisha malengo ya mradi aliyowekwa.
Post A Comment: