Na: Richard Bagolele- Sengerema
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Senyi Ngaga ametoa onyo kali kwa wazazi au walezi watakao shindwa kuwapeleka watoto wao kujiunga na kidato cha kwanza mwezi Januari 2023 kwani Serikali imejenga madarasa ya kutosha katika shule za Sekondari.
Mkuu wa Wilaya ametoa onyo hilo leo Disemba 28, 2022 wakati wa hafla ya ya makabidhiano ya ujenzi wa vyumba 152 vya madarasa ya Sekondari iliyofanyika Sekondari ya Nyampulukano katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema.
Mkuu wa Wilaya amesema hivi sasa Serikali imejenga na kuweka miundombinu ya kutosha katika shule za sekondari hivyo hakuna sababu ya wazazi kushindwa kuwapeleka watoto kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwezi Januari 2023.
"Mtoto ambaye amepangiwa kwenda kidato cha kwanza mwaka huu ni lazima aende, mtoto asipoenda shule wakati madarasa tena yenye madawati yameandaliwa huo ni uhujumu uchumi na mwaka huu lazima tutoe mfano kwa wazazi wote watakao kaidi kupeleka watoto kidato cha kwanza na ninamanisha katika hili" amesisitiza Mkuu wa Wilaya.
Mhe. Mkuu wa Wilaya mbali na kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kwa kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo kwa wakati, amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia watoto wenye uhitaji waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kwa kuwasaidia baadhi ya mahitaji ikiwemo madaftari na mahitaji mengine ya mhimu ili wote waweze kuanza masomo kwa wakati.
mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Mhe. Yanga Makaga amepongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo kwani kupitia fedha hizo zimekamilisha ujenzi wa vyumba hivyo pasipo kuchangisha fedha kwa wananchi.
Awali akitoa taarifa juu ya ujenzi wa vyumba hivyo, kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ndugu Mwita Waryuba amesema ujenzi wa vyumba hivyo ulianza mwezi Oktoba 2022, ambapo hadi sasa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ni vyumba vya madarasa 8 tu ambavyo havijakamilika kati ya vyumba 152.
Kukamilika kwa ujenzi wa madarasa hayo 152 yaliyojengwa kwa shilingi 3,040,000,000 kunaifanya Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kumaliza tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa kwa shule za Sekondari.
Post A Comment: