Na Immanuel Msumba :Monduli
Mazingira safi ni kitovu cha afya bora na maendeleo kwa wananchi. Ili kufikia lengo la kuwa na mazingira safi, ni lazima kuwa na mikakati endelevu ya kudhibiti uchafuzi wa makazi kutokana na taka zinazozalishwa kila siku.
Ili kuweka usimamizi endelevu wa usafi katika makazi ni lazima kuweka misingi ya usimamizi, tathmini na kuchukua hadhari kuhusu madhara kwa mazingira, kwa kudhibiti taka kuanzia zinapozalishwa, ukusanyaji, usafirishaji na utupwaji wake.
Wananchi wa Kitongoji cha Sinoni Kusini katika kata ya Engutoto wilayani Monduli wamemlalamikia kitendo cha uongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kuweka dampo la taka katika maeneo ya makazi ya watu na kuongeza uwezekano wa kuibuka kwa ugojwa wa Kipindupindu katika msimu wa mvua unaotarajiwa hivi karibuni.
Bi. Lucy Laizer, mkazi wa kitongoji cha Sinoni Kusini amesema kumewepo na usumbufu mkubwa kwa baadhi ya wakazi wa Kitongoji hicho. Amesema hasa wakazi wenye watoto wadogo huwalazimu kuhama nyumba kutokana kukidhiri kwa taka katika mtaa na harufu mbaya.
Pia moshi mkali huwaathiri pindi wahusika wanapochoma taka kwenye dampo hilo na huwaathiri kiafya na kusababisha vikohozi kwa watu wa mtaa huo.
Bi. Laizer ameendelea kusema baadhi ya wakazi wa kitongoji hicho wamekuwa wakiathiriwa na harufu kali na kutishia wakazi wa kitongoji hicho kupata ugonjwa wa kikohozi wakati halmashauri ikiendelea kuchoma taka katika eneo la korongo ambalo liko katikati ya makazi ya watu .
Aidha Bi Laizer alienda mbali na kuulalamikia uongozi wa halmasahauri kitengo cha usafi na mazingira kwa kusema kuwa wameshidwa kutekeleza na kuendana na kauli ya Serikali ya Awamu ya sita ya kuwataka wanachi kufanya usafi ili kuweza kujikinga na magonjwa yanayoweza kusababishwa na uchafu.
Nelson Ngoyai Lowassa ni Diwani wa Kata ya Engutoto amekiri kuwepo na tatizo hilo katika eneo la kitongoji hicho na wananchi kuadhiriwa na kadhia hiyo ambapo amesema kuwa takataka nyingi zinatupwa kwenye korongo hilo zinazalishwa na wafanyabiashara wa sokoni na wakazi wa Mji wa Monduli na kuzitupa katika korongo hilo lilipo ndani ya makazi ya watu.
Alisema dampo hilo liko kwenye viwanja vya wananchi ambao wamekuwa wakilalamika mara kwa mara lakini hadi sasa uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Monduli umeshindwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa dampo.
“Dampo hili liko kwenye viwanja vya watu na watu hawa wamelalamika kwa muda mrefu lakini halmashauri imekuwa ikituka taka hizo kwenye korongo ambalo linapitisha maji kipindi cha mvua na maji yanashindwa kwenda kwa kufuata mkondo kwa kuzuiliwa na taka na kusababisha maji kujaa kwenye makazi ya watu”.
“Kwenye vikao vyetu vya baraza la madiwani tumeshapitisha kwamba halmashauri itenge fedha kutoka kwenye mapato yake ya ndani ili tujenge dampo lakini mpaka sasa hakuna fedha yeyote iliyotengwa katika mwaka huu wa fedha wa 2022/23 hali ambayo ni hatari kwa afya za wananchi wa kata yangu.”
Anasema hivi sasa dampo hilo limekuwa kero kutokana na mvua zilizoanza kunyesha hivi karibuni kwa sababu linatoa harufu mbaya kutokana taka kuzagaa hovyo .
“Hali ni mbaya kwa sababu kutokana na tope magari ya taka hayawezi kufika kwenye korongo zinakotupwa taka hali iliyosababisha taka kuzagaa kwenye maeneo ya wananchi”.
Ngoyai anasema licha ya changamoto hiyo pia mvua zikinyesha kubwa taka hizo zinazotupwa kwenye korongo zinasafirishwa na maji ya mvua hadi kijiji cha Lashaine na kusababisha usumbufu mkubwa hali inayozua hofu ya magonjwa ya mlipuko kwa wananchi hao.
“Dampo hili siyo kero kwa kata yangu tuu ni kero hadi kwa wananchi wa Kijiji cha Lashaine ambao wakati wa mvua taka zinazosafirishwa na maji ya mvua kwenda kwenye kijiji chao na kusababisha adha kubwa “.
Anasema awali halmashauri ya Monduli ilitenga kiasi cha shilingi milioni 50 kwa ajili ya kununua eneo la kujenga dampo katika kata ya Meserani iliyopo wilayani humo.
“Halmashauri ilishanunua eneo la kujenga dampo katika kata ya Meserani ili wananchi wa kata yangu ya Engutoto waondokane na changamoto ya dampo na ninaendelea kuzungumza na Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Monduli ili fedha za ujenzi wa dampo zitengwe kutoka mapato yetu ya ndani”.
Evaresti Megiaya kutoka kata ya Monduli mjini anasema kwamba wanatozwa shilingi elfu mbili kwa mwezi kwa ajili ya gharama za kuzoa taka na kwamba anashangaa fedha hizo zinakwenda wapi zisijenge dampo.
“Tunatozwa kiasi cha shilingi elfu mbili kwa mwezi kwa ajili ya kulipia taka lakini tunashangaa kwa nini halmashauri haitengi fedha kutoka kwenye mapato yake ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa dampo licha ya eneo kununuliwa muda mrefu”.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Arusha Zelothe Steven anaeleza kuwa nimewahi kutembelea korongo hilo na nilikerwa sana na taka zilizokuwa zimesambaa kwenye makazi ya watu nasikuridhishwa na uamuzi wa Halmashauri kuacha takataka kusambaa katika eneo la makazi ya wananchi.
“Utupaji wa taka holela kiasi kile hauwatendei wananchi wetu haki ya kuishi katika mazingira bora.Uchafu wa aina ile ni hatari kwa afya za wananchi kwa sababu wanaweza kupata magonjwa ya mlipuko”.
Kutokana na kuzagaa kwa takataka katika eneo lile Mwenyekiti wa CCM anauagiza uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Monduli kuhakikisha takataka hizo zinahifadhiwa katika hali ya usafi ikiwa ni pamoja na kutafuta eneo lingine kwa ajili ya kujenga dampo mbali na makazi ya watu.
“Pia niwasihi watu wa Halmashauri wakati wakitafuta eneo la kujenga dampo wahakikishe eneo hilo linawekwa uzio kwa ajili ya kuzuia watoto kuingia pamoja na mfugo kwa sababu ni hatari kwa afya za binadamu na mifugo”.Alisema Zelothe
Mwaka jana katika viwanja vya Nyerere Square jijiniDodoma wakati Makamu wa Rais wa Jamhuri yaMuungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango akizindua Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, uzinduzi uliofanyika Makamu wa Rais alisema kazi ya kuhifadhi mazingira ikiwemo kulinda vyanzo vya maji, misitu,upandaji miti, kupendezesha miji, kufanya kusafi katika maeneo yote ya makazi na biashara, viwandani na masokoni ni lazima kuanzia sasa kuwa kazi za kudumu.
Aidha, alisema kuwa viongozi wote kuanzia ngazi ya vijiji hadi mikoa wanapaswa kusimamia uhifadhi wa mazingira na suala hilo litakuwa kipimo cha utekelezaji wa majukumu yao.
Alisema ni muhimu kuondoa nadharia katika uhifadhi wa mazingira ikiwemo kuwa na mipango isiotekelezwa bali inahitajika kazi ya ziada itakayotoa matokeo chanya katika kuhifadhi mazingira. Alisema sheria ndogondogo za uhifadhi wa mazingira zinapaswa kusimamiwa ikiwemo faini na ikiwezekana kuongeza faini hizo ili kukomesha waharibifu wa mazingira.
Alisisitiza kuwa zoezi la kutunza mazingira ni lazima kuwa shirikishi kwa wadau wote kuanzia mijini na vijijini na kuagiza wizara na taasisi zote za serikali kuhakikisha wanapanda miti.
Licha ya maagizo hayo ya Makamu wa Rais hali ni tofauti kwa wilaya ya Monduli ambapo imeshindwa kujenga dampo la kutupa taka licha ya kutengwa eneo katika kata ya Meserani.
Uwepo wa dampo hilo katika makazi ya watu limekuwa hatarishi kwa afya zao haswa watoto kutokana na watoto wengi kwenda kucheza kwenye eneo hilo ambalo halmashauri imeshindwa hata kuweka uzio kwa ajili ya kudhibiti watoto kuingia katika eneo hilo hatarishi.
Aidha taka hizo zimekuwa zikisambazwa na mbwa hadi kwenye makazi ya watu hali ambayo itishia usalama wa afya za wananchi huku baadhi wakiwa na hofu ya kupatwa na magonjwa ya mlipuko.
Post A Comment: