Na Immnauel Msumba ; Longido
UTATA umeibuka katika mabilioni ya fedha zilizotumika katika ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Longido, Arusha, bila kukamilika miaka kwa mitano iliyopita.
Pamoja na serikali kutoa Shilingi Bilioni tatu kwa awamu tokea mwaka 2018 tumebaini wananchi kukosa huduma za hospitali wilayani humo kutokana na kutokamilika kwa ujenzi kwa wakati.
Uchunguzi wetu umebaini kwamba baadhi ya wilaya nyingine za mkoa wa Arusha ambazo zilipatiwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa hosptali za wilaya zilishakamilika ujenzi na wananchi kupata matibabu yakiwemo ya kibingwa huku wananchi wa wilaya ya Longido wakilazimika kutafuta huduma nje ya wilaya hiyo na nchi jirani ya Kenya.
Wananchi wa Longido wameulalamikia uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Longido kwa kushindwa kuitisha vikao na kuwaeleza wananchi sababu zinazokwamisha kukamilika kwa hosptali hiyo ya wilaya licha ya serikali kutoa fedha.
Maiyasa Olekumbe mkazi wa wilaya ya Longido anasema amekwenda hosptalini hapo kutafuta huduma kutokana na baadhi ya huduma kutopatikana kwenye Kituo cha Afya cha Longido lakini cha ajabu amekosa huduma za matibabu kutokana na kutokamilika kwa majengo hali inayosababisha kukosekana kwa huduma.
Anasema Halmashauri hiyo ina mashine mbili za X-RAY toka 2012 na hazitumiki zipo ndani zimefungiwa na kwamba anashangaa ni kwa nini hazifungwi kwa dharura katika hosptali hiyo ili wagonjwa waweze kupata huduma badala ya kwenda mbali kutafuta huduma hiyo.
"Nimemleta mkwe wangu hapa tangu saa tatu asubuhi mpaka sasa hakuna kipimo chochote amefanyiwa cha ajabu nimeshatoa zaidi ya elfu Arobaini bila kujua mgonjwa wangu anasumbuliwa na tatizo gani baadhi ya vipimo nilivyolipia havijafanyika na nimepewa stakabadhi zilizoandikwa kwa mkono nikihoji sipati majibu".
"Pamoja na kutojua mgonjwa wangu anasumbuliwa na nini kwa sababu hakuna mashine za vipimo sasa hivi naambiwa niongeze tena hela akanunue dawa nje ya hapa na wauguzi hawataki kuniambia mgonjwa wangu anasumbuliwa na nini".
Neema Laizer ni mkazi wa Longido na anaipongeza serikali kwa kutoa fedha nyingi sana kwa ajili ya ujenzi hospital ambapo Awamu ya kwanza ilikuja Bilioni Moja na milioni mia tano,awamu ya pili milioni 300,Milioni 800 Awamu ya tatu na Milioni 500,huku mapato ya ndani yakiwa Milioni 300 sambamba na milioni 61 kutoka kwa wahisani wa uwindajii kwa ajili ya Ujenzi wa Hospital ya Wilaya ya Longido lakini anasema kuna changamoto nyingi zimeukumba Ujenzi wa Hospital ya Wilaya ikiwemo kutokukamilika kwa majengo mengi kwa muda mrefu kwa zaidi ya miaka minne.
"Mpaka sasa pale yamekamilika majengo mawili tu kwa asilimia mia moja ndani ya majengo 17 ambayo ni Jengo la nyumba ya Watumishi na jengo la mionzi (X-RAY),pamoja na jengo la OPD ambalo limeanza kutoa huduma kwa wiki hii, Halmashauri yetu ya Longido ilipewa fedha sawasawa na Halmashauri nyingine na wamekamilisha muda mrefu sana kwa nini hii kwetu iko hivi mpaka sasa"
"Halmashauri yetu imetoa zaidi ya milioni mia tatu katika mapato yake ya ndani ili kuweza kukamilisha ujenzi wa majengo haya lakini bado hali ni ile ile,kuna mashine ya X-RAY ipo pale jengo lipo lakini haifanyi kazi hususani kule Kituo cha Afya kuna X-RAY mashine nyingine ipo tokea 2012 lakini haifanyi kazi ukiuliza utaambiwa wataalamu wa kuitumia hamna tunateseka inabidi tuendee kutibiwa Arusha kwenye Hospital ya Rufaa ya Mkoa ya Mount Meru na za binafsi" Alisema na kuongezea
"Nilijaribu kuzungumza na Diwani wangu akaniambia kila siku serikali inaleta fedha pale kwa ajili ujenzi wa majengo mengine mapya lakini wakiwauliza wataalamu kwanini wasiandike barua kwa Katibu Tawala Wilaya ili kuomba kubadilishiwa matumizi ya fedha ili ikamilishe majengo ya awali yawe hata kumi lakini yawe yanatoa huduma maana wanachi wa longido ni wachache na majengo yanavyojengwa mengi hatutaweza kuyatumia yote aliniambia wataalamu wanasema fedha zote zinakuja na maelekezo na hazitakiwi kuombewa kubadilishwa" Alisema pia
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Longido Simon Oitesoi amesema kwamba ujenzi wa Hospitali ile unasuasua sana kwani kuna majengo ambayo hayajakamilika ila ni matarajio yao kuwa Jengo la OPD linafanya kazi kwa sasa,
"Ni kweli kuna majengo yameanza kujengwa toka 2018 na mimi nimeyakuta hivyo yanamapungufu mengi sana hayajakamilika mpaka leo hii ambayo ni zaidi ya majengo manne,tumeamua kuchukua makusanyo ya ndani ili tukaangalie kama tutaweza kukamilisha majengo gani ili yaweze kuanza kutoa huduma"
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido Stephen Anderson Ulaya anasema ni kweli wana upungufu wa watumishi wa mionzi (X-RAY) na kwamba wakati anasubiri wataalamu kutoka serikalini ameamua kuchukua watumishi wawili wa idara ya Afya na kuwapeleka kwenye mafunzo ya muda mfupi ili wakirejea waweze kutoa huduma za mionzi na ziweze kuanza katika hosptali hiyo.
Post A Comment: