Kwa mujibu wa Ndejembi, hali hiyo ilisababishwa na maofisa utumishi na hicho ni kielelezo namna wanavyokwamisha stahiki za watumishi wa umma.
Akisimulia mkasa huo juzi jijini hapo kwenye Mkutano Mkuu wa Nusu Muhula wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Chamwino, Ndejembi alisema kuna wakati Ofisi ya Rais (Utumishi) inatupiwa lawama kuhusu stahiki za watumishi wa umma yakiwamo malimbikizo ya mishahara, chanzo kikubwa ni ngazi za chini hasa wilayani.
“Changamoto iliyopo kama kuna madeni ya mishahara hayajafikishwa Ofisi ya Rais Utumishi, wakati mwingine yanawasilishwa bila viambatanisho na unapokwenda kwenye uhakiki pale halmashauri inajulishwa kuchukua ili kufanyia kazi, hayachukuliwi sijui kwa Chamwino,” alisema.
Alisema suala la malimbikizo ya mishahara huwa linampa uchungu sana kutokana na alivyosota kwa miaka minne akifuatilia mishahara yake ya ukuu wa wilaya ya miezi minne.
“Hili limewahi kunikuta na mimi. Niliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya mwaka 2016. Nilikaa miezi minne bila mshahara. Baada ya kupata ‘cheque number’ mwezi uliofuata mshahara haukuingia, nilienda Julai nilikuja kulipwa mshahara Novemba.
“Maofisa utumishi waliniambia usijali fedha zote zitakuja. Baada ya muda nikaambiwa kuna fomu natakiwa kujaza, nikajaza lakini kale kakiwango nilichoona kwenye kompyuta kalikuwa kazuri, niliwauliza lini wakasema muda si mrefu utalipwa. Nimekaa hadi nimeachia ukuu wa wilaya mwaka 2020 kwa hiari ili kupambana na wajumbe jimboni.
“Niliachia Julai, 2020 lakini kabla ya wiki mbili hivi niliuliza deni langu vipi la mshahara, kumbuka limepita miaka minne sijalipwa, wakati jibu hili deni lako lipo tayari kulipwa na kwamba limepita hatua zote linalipwa,” alisema.
Ndejembi alibainisha kuwa aliambiwa litalipwa muda wowote akaamini fedha hizo zitamsaidia mafuta kuzunguka kufanya kampeni kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2020.
“Niliposhinda kura za maoni nimetoka hali mbaya nikakumbuka si ninadai, nikaenda tena nilipofika nikaambiwa inabidi ujaze fomu nyingine kwa kuwa uko nje ya ‘payrol’ (mfumo wa malipo). Nikasema sawa, nikajaza na nikaambiwa italipwa haraka nikapata matumaini,” alisema.
Kwa mujibu wa Ndejembi, aliposhinda uchaguzi alirudi tena mkoani (Dodoma) kudai fedha zake, lakini wakamwambia sasa amerejea kwenye orodha ya malipo ya mshahara, hivyo namba yake itatumika ile ile na kutakiwa kujaza fomu nyingine.
“Nikajaza fomu nimekaa muda mrefu hadi kuapishwa ubunge. Nikaenda tena nikaambiwa sasa deni lako limeiva, nikaambiwa liko Hazina. Hiyo ilikuwa Desemba 4, 2020. Siku hiyo nilikuwa na muda nikatoka nikaenda Hazina, nikamwona Katibu Mkuu nikamwambia, akaitwa anayehusika kama mnavyojua mshahara wa ukuu wa wilaya kwa miezi minne.
“Ile kuangalia kwenye mfumo nikaambiwa hakuna deni lolote na nikashuhudia hakuna nyaraka yoyote ya deni langu. Nikampigia simu Ofisa Utumishi aliyeniambia nikamwambia halipo, mara litakuwa utumishi halijafikishwa Hazina.
“Desemba 5, 2020 nikiwa Dar es Salaam, Baraza la Mawaziri likatangazwa. Mungu akanijalia nikapelekwa kuwa Naibu Waziri Utumishi. Cha kwanza nikakumbuka deni langu na mimi jana yake nilikuwa nimeambiwa deni liko Utumishi. Nimefika ofisini nikamwambia Katibu Mkuu nina madai ya mishahara yangu miezi minne, wakaingia kwenye mfumo deni halijawahi fika Utumishi,” alisema.
Naibu Waziri alisema deni hilo halikuwahi kufika Ofisi ya Rais Utumishi licha ya kujaza fomu mbalimbali.
“Mara nyingi Ofisi ya Rais Utumishi inapewa jina baya au serikali kuu kuonekana haijali watumishi lakini madeni yamekwamishwa huko hayafiki eneo linalotakiwa kufika,” alisema.
Ndejembi alisema serikali inatoa fedha nyingi kulipa madai ya watumishi kutokana na umuhimu wao lakini wapo watu wanaokwamisha jitihada hizo.
Aliwahikishia watumishi na walimu kuhusu malimbikizo ya mishahara atakuwa anafuatilia kwa karibu kwa kuwa ana mkasa nalo.
Post A Comment: