Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano, Dk Selemani Jafo (kulia)akizindua Chama cha Bioteknolojia Tanzania (BST), katika Mkutano Mkuu uliofanyika katika Ukumbi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu, Dares Salaam
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Suleiman
Jafo amewataka watafiti na wataalamu waliojikita kwenye teknolojia ya
bioteknolojia kufanya tafiti ambazo zitawezesha jamii kupata uelewa na kuondoa
hofu iliyopo kuhusu teknolojia hiyo.
Waziri Jafo alisema hayo jana kwenye ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa Chama
cha Bioteknolojia Tanzania (BST) uliofanyika katika ukumbi wa Tume ya Sayansi
na Teknolojia (COSTECH) jijini Dar es Salaam.
Dk Jafo alisema kumekuwa na mkakanganyiko kuhusu bidhaa zinazotokana na
bioteknolojia hapa nchini, hivyo njia ya kuondoa hali hiyo ni vema watafiti
wakafanya tafiti za kina ambazo zitaiwezesha Serikali kuchukua hatua stahiki.
Alisema taarifa zinaonesha bioteknolojia inatumika kwenye sekta ya afya,
viwandani, kilimo na kwingineko ila upingaji au uungaji mkono umejikita katika
kilimo hali ambayo inaibua malumbano kila kukicha.
“Sisi Serikali hatuna shida na tafiti kuhusu bioteknolojia, ila msukumo
mkubwa utaonekana iwapo tafiti zitafanyika ili kuhakikisha kundi ambalo
linapinga ua halina uelewa liweze kuelewa, kwani haiwezekani hata nguo ambazo
tunavaa zinatoka na bioteknolojia, lakini wapo watu wanapinga, lazima elimu ya
kutosha itolewe,” alisema.
Waziri Jafo alisema wapo watu ambao wanahusisha bioteknolojia na masuala ya mabadiliko ya
tabianchi yaliyopo kwa sasa, hivyo yote hayo ili kuondoa hiyo dhana tafiti na
elimu ni muhimu.
Alisema wizara na serikali kwa ujumla wanasubiri maazimio ya BST katika
eneo hilo la bioteknoloji, ili iangalie ni njia gani ya kwenda nayo kwa maslahi
ya taifa.
“Naahidi kutoa ushirikiano BST kuhakikisha wananchi wanapata uelewa ili
nchi isonge mbele kibiashara, kiuchumi na kijamii,” alisema.
Waziri Jafo alisema pamoja na ukweli kuwa bioteknolojia inahusisha sekta
nyingi ila BST inajukumu kutoa elimu katika eneo la kilimo ambalo limekuwa
likipigiwa kelele, hasa kwa kueleza faida na hasara zilizopo.
inapaswa kuwaelimi wananchi kwa kulinganisha aina ya kilimo kimoja na
kingine cha ndani na cha nje ya nchi.
“Nchi kama China, India na nyingine ambazo zina watu wengi zina zinazalisha bidhaa zinazotokana na bioteknolojia, hivyo watafiti na watalaamu wakitumia mifano hiyo na kuwaweka sawa wananchi wanaweza kuelewa na kuimarisha kilimo hicho,”alisema.
Jafo alisema historia inaonesha bioteknolojia ilianza tangu karne ya 19
kwenye ‘Tissue Culture’ hivyo sio jambo geni na kwamba elimu ndio njia
itakayoweza kuondoa hofu iliyopo.
Alisema Serikali ina sera ya mazingira ya mwaka 1997 ambayo ilikuwa na
kasoro kidogo na kufanyiwa marekebisho mwaka 2021 na sera mpya ya mazingira
iliyozinduliwa rasmi mwaka 2022.
Pia alisema ipo sera inayozungumzia bioteknolojia, hivyo ikitumika
inavyopaswa itakuwa njia sahihi ya kufikisha elimu kwa jamii.
“Sera ya kilimo ya mwaka 2015 nayo inazungumzia jinsia gani mchakato wa uangalizi wa kimazingira na bioteknolojia
unavyokwenda sambamba katika kusimamia maendeleo ya nchi,” alisema.
Awali akizungumza kwenye mkutano huo wa kwanza wa Mwenyekiti wa BST,
Profesa Peter Msolla alisema, matumizi ya bioteknolojia duniani yameleta
manufaa makubwa kwenye sekta mbalimbali kama kilimo, afya, mifugo, viwanda na
mazingira.
“Bioteknolojia imewezesha uzalishaji wa miche isiyo na vimelea vya
magonjwa, mazao bora yasiyoshambuliwa na
visumbufu vya magonjwa na wadudu, pamoja na kupunguza gharama za
uzalishaji.
Katika sekta ya afya imerahisisha utambuzi wa magonjwa kwa usahihi, pamoja
na utengenezaji wa chanjo na dawa mpya na zenye ubora zaidi kukabili magonjwa
sugu kwa mfano insulin kwa wagonjwa wa kisukari, homa ya ini (hepatitis B),
saratani ya shingo ya kizazi, magonjwa ya kuhara kwa watoto, na chanjo za
VVU/Ukimwi na Uviko-19,” alisema.
Alisema utafiti unaendelea wa kutumia teknolojia hiyo katika kuzuia au
kutokomeza ugonjwa wa malaria.
Prof Msola alisema hali kama hiyo imeonekana kwenye sekta ya mifugo kwa kurahisisha utambuzi wa
magonjwa kwa usahihi, kuongeza uzalishaji wa aina bora za mifugo, pamoja na
utengenezaji wa dawa na chanjo;
“Katika sekta ya viwanda bioteknolojia imeweza kuongeza ufanisi na tija
katika kutengeneza bidhaa mbalimbali za vyakula, pamoja na madawa na kemikali
kwa matumizi ya kilimo na viwandani bila kuharibu mazingira.
Katika sekta ya mazingira imechangia kuhifadhi au kuboresha mazingira kwa
kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya viuatilifu na kubaini mbinu bora za
kutambua, kuzuia na kusafisha sumu katika mazingira na kubadilisha taka za
mashambani na viwandani kuwa mbolea na gesi,” alisema.
Alisema BST imebaini kuwa uelewa na ufahamu wa baadhi ya wadau kuhusu matumizi
ya bidhaa zitokanazo na bioteknolojia ya kisasa (GMO) ni mdogo hali ambayo
imesababisha ongezeko la taarifa zisizo sahihi kuhusu teknolojia hiyo na zenye
kuleta hofu kwa jamii ya Watanzania.
Mwenyekiti huyo alisema baadhi ya wanasiasa na hasa wabunge wamekuwa na
mashaka na wasiwasi juu ya matumizi ya bioteknolojia ya kisasa katika sekta ya
kilimo, ingawa wanakubali kwa urahisi matumizi yake katika sekta ya afya.
Aidha, Msola alimpongeza Dk Jakaya Kikwete kwa kutunukiwa Tuzo ya Shujaa wa
Bioteknolojia Tanzania kutokana na mchango wake mkubwa katika kuendeleza
uvumbuzi wa teknolojia za kisasa ili hatimaye ziwanufaishe wakulima na taifa letu kwa ujumla.
“Tuzo hiyo ilitolewa na Wakfu ya Teknolojia za Kilimo Afrika (African
Agricultural Technology Foundation, AATF) iliyoko Nairobi-Kenya kupitia mradi
wake wa Jukwaa la Bioteknolojia za Kilimo Afrika (OFAB),” alisema.
Alisema Kikwete alifanikishwa kurekebisha na kuridhia kanuni za matumizi
salama ya bioteknolojia ya kisasa na hivyo kuwezesha nchi kufanya utafiti wa
mahindi yanayostahimili ukame na bungua wa mahindi.
Pia aliwezesha utengenezaji, uwekezaji na uzinduzi wa maabara mahiri ya
bioteknolojia ya kisasa kwenye kituo cha utafiti TARI-Mikocheni, Dar es Salaam.
“Hii iliwezesha utafiti wa kijenetiki ili kuzalisha mihogo inayostahilimi
magonjwa, hususan batobato na michirizi kahawia. Maabara hii ilivutia watafiti
na wanataaluma kutoka nchi mbalimbali za Afrika waliokuja kufanyia utafiti wao
TARI-Mikocheni,” alisema.
Msola alisema Kikwete alikuza ushirikiano na nchi zinazotuzunguka katika kuendeleza bioteknolojia ya kisasa hususan dhidi ya magonjwa na wadudu waharibifu katika kilimo. “Yeye alitambua fika kwamba haya maadui wa uzalishaji katika kilimo hayana mipaka,” alisisitiza.
Post A Comment: