Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Ikwambi kata ya Mofu tarafa ya Mngeta Wilaya ya Kilombero wanadaiwa kuchoma moto ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Mofu kutokana na kutoridhishwa na maamuzi yanayotolewa na viongozi wakati wa utatuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji.
Akizungumza na Mwandishi wetu mwenyekiti mstaafu wa Kijiji cha Ikwambi, Victor Timbulu amesema tukio la uchomaji moto la ofisi hiyo limesababisha vifo vya watu wawili ambao mpaka sasa miili yao ipo kwenye eneo la tukio ikisubiri polisi huku Diwani wa kata ya Mofu, Greyson Mgonera akiwa amejeruhiwa vibaya maeneo mbalimbali ya mwili wake.
Amesema jana viongozi wa Kijiji na kata wakiwa kwenye kikao wananchi walifanya maadamano hadi kwenye ofisi hiyo na kuchoma moto huku wakilalamika viongozi kuwapendelea wafugaji na kwamba kila wanapopeleka malalamiko hakuna hatua zozote zinazochukuliwa.
"Juzi wakulima kama kumi walipigwa na wafugaji na ilitolewa taarifa kituo kidogo cha polisi lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa," amesema Timbulu
Amesema jana asubuhi wananchi baada ya kutokea hilo wakavamia ofisi na kuwafunga kamba wenyeviti wawili wa vitongoji vya Igia na Milamila baadae kumfuata mwenyekiti wa Kijiji kanisani na kumfunga kamba, ambapo baadaye walimfuata kituo cha polisi kata hiyo naye kukamatwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Hanji Godigodi alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kwamba miili ya waliouawa iko eneo la tukio na yeye alikuwa akielekea kwenye eneo hilo.
Godigodi amesema watu tisa wanashikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo.
Mkuu huyo wa Wilaya anasema wananchi wametumia silaha za jadi na sababu za kutokea tukio hilo ni wakulima kulalamika wafugaji kutochukuliwa hatua.
"Wakulima na wafugaji wamekuwa na tabia ya kulipana wao kwa wao bila kufuata taratibu na hiyo inakuwa hakuna kesi, kinachotakiwa ni wao kufungua ili hatua zichukuliwe,"amesema.
Post A Comment: