wizarahmth Mkurugenzi Msaidizi wa Usalama Mtandao wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Steven Wangwe akimkabidhi t-shirt Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) Macrise Mbodo yenye ujumbe wa mwezi wa elimu ya usalama mtandao alipotembelea banda la maonesho la Wizara hiyo wakati wa kongamano la Biashara Mtandao na Anwani za Makazi lililofanyika leo Oktoba 8, 2022 jijini Dar es Salaam.
Posta masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania akifungua Kongamano la Biashara mtandao na Anuani za Makazi lilioandaliwa na Shirika hilo na kufanyika Leo Jumamosi oktoba 08 , 2022 katika ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bi. Teddy Njau akisalimiana na Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Macrice Mbodo wakati wa Kongamano la Biashara Mtandao na Anwani za Makazi kuelekea Siku ya Posta Duniani ambapo kilele chake ni tarehe 9 Oktoba 2022 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, tarehe 08 Oktoba, 2022.
***************************
Na Faraja Mpina, WHMTH, DAR ES SALAAM
SERIKALI kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inaendelea kuhakikisha inaimarisha usalama wa huduma zinazotolewa kwa njia ya mtandao ikiwa ni pamoja na biashara mtandao ili wananchi waendelee kunufaika na mapinduzi ya teknolojia yanayoendela kutokea nchini.
Hayo yamezungumzwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Usalama Mtandao wa Wizara hiyo, Mhandisi Steven Wangwe wakati wa kongamano la Biashara Mtandao na Anwani za Makazi lililofanyika leo Oktoba 8, 2022 jijini Dar es Salaam kuelekea maadhimisho ya siku ya Posta Duniani Oktoba 9,2022.
“Mwezi Oktoba kila mwaka duniani ni mwezi wa kujenga uelewa na kuelimisha umma kuhusu masuala ya usalama mtandao leo tupo kwenye kongamano la biashara mtandao hivyo ni vema tukumbushane matumizi salama ya mtandao”, Amezungumza Mhandisi Wangwe.
Ameongeza kuwa lengo ni kupunguza matukio ya uhalifu mtandaoni kwa kujenga uelewa kuhusu mbinu zinazotumika kufanya uhalifu mtandaoni, namna wanavyoweza kubaini mashambulizi ya mtandao na masuala gani wanayoweza kufanya ili kujikinga dhidi ya uhalifu wa mtandao.
Mhandisi Wangwe amesisitiza wananchi kujiridhisha kabla ya kufungua au kupakua chochote mtandaoni, kulinda taarifa binafsi na nambari ya siri (PIN), kusasisha vifaa vya TEHAMA na program tumizi mara kwa mara ili kupunguza mianya ya udukuzi na wahalifu wa mtandao kuingilia programu au vifaa husika.
Sambamba na hayo ametoa rai kwa wananchi kuchukua tahadhari kwa kuacha kutumia Wi-Fi za bure zisizohitaji kuingiza nywila (Password) pamoja na kuendelea kuripoti matukio ya uhalifu kupitia namba 15040.
Kwa upande wa Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Macrise Mbodo amesema kuwa mifumo ya biashara mtandao ya shirika hilo kupitia huduma yake ya duka mtandao ni salama na kuwasihi wafanyabiashara kutumia fursa hiyo kutangaza biashara zao na kupata masoko ya bidhaa wanazouza.
Aidha, amezungumzia Kongamano la biashara mtandao na Anwani za makazi ni sehemu ya kujadili wapi tulipo na tunapokwenda kwa kuangazia maeneo yanayotakiwa kuboreshwa ili Taifa lifanye vizuri zaidi katika biashara mtandao.
Kauli mbiu ya mwezi wa usalama mtandao kwa mwaka 2022 inasema kuwa “Usalama Mtandao huanza na mtu Binafsi”.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
Post A Comment: