Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro imeendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa kuhakikisha kwamba, wanatoa mikopo itokanayo na asilimi 10 ya mapato ya ndani, kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.


 Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mwanga Mhe.Salehe Mkwizu amekabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi Milioni 122,767,000/=, kwa jumla ya vikundi 15 huku aki warai wanavikundi hao kufanya marejesho kwa wakati.



"Fedha hizi ni sehemu ya manufaa ya urejeshaji mzuri unaofanywa na vikundi ambavyo, vikipewa fedha vinarejesha vizuri na kwa wakati,na mimi nitoe raia kwa wanufaika wa mikopo hii kuhakikisha kwamba, fedha mnazopatiwa mnakwenda kuziingiza kwenye miradi mliyo ombea fedha na siyo kuzifanyia kazi ambayo haikukusudiwa" alisisitiza Mkwizu.


Mkwizu alibainisha kuwa  fedha hizo zinapaswa kurudi kwa wakati ili vikundi vingine vikopeshwe, pia nao waendelee kukopeshwa mara nyingi zaidi kadri ya watakavyokuwa wanarejesha. 



Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Bi. Mwajuma Nasombe, amewaomba Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri kuhakikisha kwamba, wanasimamia vizuri vikundi vyao ili warejeshe mikopo hiyo kwa wakati, na vikundi viendelee kukopa zaidi.


 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga imekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambapo katika mwaka wa fedha wa Serikali 2021/2022, Halmashauri ilifanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya Tsh. 481,572,500/= kwa jumla ya vikundi 70.

Share To:

Post A Comment: