Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati Dodoma, John Mwanja akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa chuo hicho kwa Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) Neema Mwakalyelye (kushoto), wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja ya kukagua ujenzi wa chuocha VETA wilayani Ikungi mkoani hapa juzi. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro.

Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) Neema Mwakalyelye (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Ikungi. Kutoka kulia waliosimama mbele ni ni Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Ikungi, Erick Nyoni, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida,Widege Mzalendo, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi,Jerry Muro, Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Mika Likapakapa na Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati Dodoma, John Mwanja. Waliosimama nyuma kutoka kushoto ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ikungi (OCD) Suzana Kidiku na kushoto kwake ni Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Winfrida Funto.

 

Na Dotto Mwaibale, Singida

 

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi nchini na kutoa fedha za miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyuo vipya na uboreshaji wa vyuo vya zamani.

 

Pongezi hizo zimetolewa juzi na Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati Dodoma, John Mwanja mbele ya Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) Neema Mwakalyelye kwa niaba ya mkurugenzi mkuu wa VETA wakati wa kikao na viongozi mbalimbali wa wilaya ya Ikungi cha kupata taarifa ya ujenzi wa chuo cha ufundi VETA kilichojengwa wilayani humo na VETA Kanda ya Kati-Dodoma kwa usimamizi wa TAKUKURU.

Aidha Mwanja alitoa shukurani hizo za dhati kwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Neema Mwakalyelye kwa usimamizi thabiti katika shughuli za serikali hivyo kuifanya serikali ya Awamu ya sita ing’are katika kuwaletea wananchi maendeleo yao.

 

Katika hatua nyingine Mwanja alitoa shukrani kwa uongozi wa chama na serikali wa  Mkoa wa Singida na Wilaya ya Ikungi kwa ushirikiano wao mkubwa wanaowapa katika kutekeleza mradi huo wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Ikungi.

 

Akizungumzia faida ya chuo hicho mara kitakapokamilika alisema kinatarajiwa kuhudumia wakazi wapatao 343,985 wa Wilaya ya Ikungi na wakazi  wapatao  1,754,370  wa  Mkoa  wa  Singida.  Pia,  wakazi  wa  mikoa  jirani  watanufaika  na huduma za chuo.

.

Alisema katika utaoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwenye kozi za muda mrefu na kozi za muda mfupi,  chuo  hicho kitajielekeza  katika  kutoa  mafunzo  kwenye  maeneo  ya  kimkakati  kulingana  na mahitaji ya shughuli za kiuchumi wanazofanya wananchi wa Wilaya ya Ikungi na Mkoa wa Singida kwa ujumla.

 

Alisema katika kutekeleza mradi huo VETA imekumbana na changamoto mbali mbali kama

kupanda  kwa  bei  ya  vifaa  vya  ujenzi  wakati  wakiendelea  na  utekelezaji  wa  mradi,  hali iliyopelekea  pesa  iliyotengwa  kutokidhi  mahitaji  halisi  ya  mradi  kutokana  na  bei  za  vifaa kupanda zaidi ya matarajio ya awali.

.

Alitaja changamoto nyingine waliyokumbana nayo ni uwezo mdogo wa kiuchumi wa mafundi waliowatumia hivyo kupelekea kushindwa kuwalipa vibarua wao kwa wakati na kupelekea baadhi yao kuacha kazi, hivyo kupelekea kuchelewa kwa utekelezaji wa mradi.

 

“Sisi watumishi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) husunani  VETA Kanda ya Kati tunaahidi kuendelea kutekeleza mradi huu na mingine yote kwa uadilifu mkubwa, na kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu, miongozo na maelekezo mbalimbali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” alisema Mwanja.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: