NA DOTTO KWILASA, DODOMA 

UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT)umempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan  kwa hatua ya kushinda tuzo ya kipekee ya amani duniani iliyotokana na Uongozi wake mahiri uliotukuka na kumtaja kuwa ni Rais pekee mwanamke Afrika kupata tuzo hiyo.

Akiongea na waandishi wa habari leo jijini hapa Mwenyekiti wa UWT-Taifa Gaudensia Kabaka amesema kutokana na uongozi mzuri wa Rais Samia umepelekea Kurugenzi ya Jumuiya ya kimataifa ya watetezi wa amani kumtangaza kuwa mshindi wa tuzo ya dhahabu ya malengo ya maendeleo endelevu na  tuzo ya kipekee ya amani duniani .

Amesema,tuzo hizo mbili zimetokana na juhudi zake katika ujenzi ,uboreshaji wa miundombinu ya  afya na elimu ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wake katika kueneza amani kwa watanzania  na uhuru wa kisiasa na kuabudu.

"Sote tunafahamu kuwa Rais samia ni balozi wa amani ambapo amekuwa alifanya yote haya kwa vitendo mfano mzuri ni pale alipowasamehe wafungwa wa kisiasa na kuweka mazingira ya kuwa karibu zaidi na vyama vya upinzani hapa nchini,tuzo hii inamstahili,"amesema

Amesema,tuzo hiyo ni fahari kwa UWT na wanawake wote nchini kwa kuwa itakwenda kuchochea ari na nguvu ya mwanamke katika masuala ya uongozi jambo litakalozidi kuandika historia duniani.

"Ifahamike kuwa hili ni jambo la kipekee kwani kwa Afrika marais waliowahi kupokea tuzo hii ni watatu akiwemo Rais George Wear wa Liberia, Rais Seretse Ian Kham wa Botswana na sasa ni zamu ya Tanzania kupitia Rais Samia, "amesema

Sambamba na hayo Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa Kurugenzi hiyo pia ambayo ipo chini ya umoja wa mataifa (UN)imetambua Rais Samia anavyojali masuala ya usawa wa kijinsia kwani ameteua wanawake wengi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ambapo Tanzania inaongoza kwa bara la Afrika. 

"Kurugenzi hiyo imeangalia zaidi katika uongozi wa Rais Samia kutimiza lengo namba tatu la afya njema na ustawi wa jamii, lengo la nne ni utoaji wa elimu bora ambapo mama Samia amejenga madarasa ya kutosha kwa shule za msingi na sekondari pia anaendelea kutoa elimu bila malipo nasi tupo nyuma yake kwa kila hatua,"amesisitiza Kabaka.

Pamoja na hayo ametumia nafasi hiyo kueleza mafanikio mengine katika Serikali anayoongoza Rais Samia kuwa ni pamoja na kuweka usawa kijinsia na kufafanua kuwa suala hilo limedhihirishwa vyema kupitia nafasi zake nyingi za uteuzi anazozifanya kwa kuwaweka wanawake wengi.

"Kupitia yeye (Samia)wanawake sasa wanekuwa vinara wa uongozi katika nafasi mbalimbali zikiwemo za ukuu wa mkoa,ukuu wa Wilaya, makatibu tawala,Wakurugenzi, makatibu wakuu wa Wizara na wenyeviti wa bodi mbalimbali, "amefafanua mwenyekiti huyo wa UWT. 

Katika hatua nyengine Kabaka ameeleza kuwa umoja huo wa wanawake unatambua jitihada nyingi hata ambazo hazizungumzwi mara kwa mara na kueleza jitihada za Rais Samia katika kuondoa njaa kwa kuhakikisha kuna akiba ya chakula chankutosha ,usalama wa chakula na lishe kwa watanzania.

Kabaka amesema,"Tumeshuhudia namna Rais wetu akisaini mkataba wa usimamiaji wa shughuli za lishe ,sambamba na hayo amepunguza gharama ya kununua mbolea kwa ajili ya kilimobili wananchi wake washiriki vyema kulima na kupata mazao bora,lazima tuhakikishe tunamlinda na kusimama nae kwa kila hatua ,"amesema.

Share To:

Post A Comment: