Na Gift Mongi,Moshi
Mwanzo wa elimu na kufikia malengo sii ngazi ya kidato cha nne pekee bali wahitimu katika ngazi hiyo wanatakiwa kuwa na shauku ya kufika mbali kimasomo kwa lengo la kuijenga nchi lakini pia kutoa msaada kwa jamii inayowazunguka.
Katika kufikia malengo hayo ni dhahiri shahiri kuwa wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne wanatakiwa kujiwekea malengo ya mbali zaidi ili kuleta mafanikio katika taifa kupitia taaluma zao.
Akizungumza katika mahafali ya 16 ya shule ya sekondari Himo iliyopo halmashauri ya Moshi mkoani Kilimanjaro mwenyekiti wa umoja wa vijana wa chama cha Mapinduzi, (UVCCM) wilaya ya Moshi vijijini, Yuvenal Shirima amesema ipo haja ya wahitimu kubadilika bfikra na kuangaza fursa mbalimbali katika kulisaidia taifa.
"Kufika kidato Cha nne haitoshi bali mnatakiwa kuwaza mbali zaidi ya hapa lakini niwasihi mjiandae vyema na mitihani ya kitaifa ilioko mbele yenu kwani hapa mlipo ndiyo mwanzo wenu wa kuzifikia ndoto zenu kimaisha"amesema Shirima
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo ni kuwa ili wahitimu hao waweze kufikia malengo yao ya kimaisha ni lazima wasome kwa bidii ili waweze kufaulu katika mitihani yao ya mwisho na kuendelea na hatua nyingine za kielimu, ambapo pia amewaasa wazazi kuwalea watoto katika misingi iliyo bora, ikiwa ni pamoja na kuepuka kuwafanyia vitendo vya kikatili.
"Nisiishie hapa naomba kuwakumbusha wazazi na walezi kuwa ipo haja ya kukaa na vijana wetu vizuri lengo likiwa ni kuepusha kutoelewana ambapo mwishowe ni ukatili wa kijinsia ila mmejitahidi kuwakea hadi hapa mlipofikia kwani wanaenda kufanya mitihani yao bila vikwazo vyovyote vile"aliongeza.
Katika hatua nyingine mwenyekiti huyo ambaye ameahidi kurekebisha darasa Moja kwa kulifanyia ukarabati na Kutoa mashine ya kuchapa(printer)moja shuleni hapo, pia amempongeza rais na mwenyekiti wa CCM Samia Suluhu Hasani kwa kazi nzuri anayofanya ikiwemo kuwezesha kujengwa madrasa manne katika shule hiyo.
Kwa upande wake Zablon Mhadisa ambaye ni mkuu wa shule hiyo alizitaja baadhi ya changamoto zilizopo shuleni hapo kupitia taarifa yake kuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo uhaba wa maabara moja.
Akabainisha kuwa pia kuna uchakavu wa miundombinu ya madarasa matano, pamoja na uhaba wa vifaa vya maktaba na kuwa vikikamilishwa huenda ufaulu kwa wanafunzi ukaongezeka tofauti na matokeo ya miaka ya nyuma
Mmoja wa wazazi wenye wahitimu shuleni hapo Gervas Munuo amesema kwa sasa serikali imejipanga kuinua kiwango cha elimu na wadau wa elimu hawana budi kuunga mkono ili kufikia malengo ya serikali katika kupambana na ujinga maradhi na umaskini.
Post A Comment: