Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya kimataifa ya kuhudumia makontena Tanzania katika bandari ya Dar es Salaam (TICTS) imeisababishia taifa hasara kubwa baada ya kudondosha makontena matatu baharini na kusababisha meli kushindwa kushusha mafuta kwa siku kadhaa.
Tukio hilo lililotokea wiki iliyopita ni miongoni mwa mlolongo wa tuhuma za uzembe na ukosefu wa ufanisi wa TICTS ambayo imekuwa ikisimamia eneo la makontena la bandari ya Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka 20 bila tija.
"Kutokana na uzembe huo mkubwa wa TICTS wa kudondosha makontena hayo baharini, meli zilishindwa kuingia eneo la kupakulia mafuta yanayoingia nchini (KOJ) Kurasini jiji Dar es Salaam kwa siku tatu nzima," alisema mdau mmoja wa bandarini.
"Hasara kwa taifa kwa meli za nje kushindwa kushusha mafuta nchini kwa siku tatu ni kubwa mno. Huu uzembe wa TICTS hauwezi kuvumilika."
Njia ya meli kuingia Kurasini kupakua mafuta ilifunguliwa juzi baada ya makontena hayo matatu kuopolewa bandarini.
Serikali ya Tanzania kwa sasa iko kwenye majadiliano na TICTS kuhusu kuongeza au kutoongeza mkataba wake, huku kampuni hiyo ikilaumiwa na wadau wa biashara na usafirishaji kwa kukosa ufanisi.
Serikali hivi karibuni iliongeza mkataba wa TICTS kwa miezi mitatu tu ili kuruhusu majadiliano hayo kukamilika.
Wadau wa sekta za biashara na usafirishaji wameitaka serikali kutoipa kampuni ya TICTS mkataba mpya wa kuendesha eneo la kontena la bandari ya Dar es Salaam kwa kushindwa kufikia lengo la kuongeza wingi wa mzigo kwa asilimia 37 kwa mwaka na kushindwa kuwekeza kwenye miundombinu ya bandari.
Chama cha siasa cha ACT-Wazalendo nacho kilijitosa kwenye sakata hilo la TICTS na kuitaka serikali kutoongeza mkataba wake ili kunusuru uchumi wa taifa.
Kusuasua kwa TICTS kumeongeza gharama ya kuingiza mizigo nchini na kulikosea taifa mapato ya trilioni ya Shilingi kutokana na wafanyabiashara wa nchi jirani kuamua kuikwepa bandari ya Dar es Salaam na kukimbilia bandari za Kenya, Afrika Kusini na Namibia zenye ufanisi zaidi.
TICTS walipewa nyongeza ya mkataba wa miaka mitano mwaka 2017 baada ya kushindwa kuleta ufanisi tangu wapewe kuendesha eneo la kontena la bandari ya Dar es Salaam zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Kuna juhudi zinaendelea ili TICTS waongezewe mkataba mwingine wa miaka mitano licha ya kushindwa kuleta ufanisi kwa zaidi ya miaka 20.
Takwimu za serikali zinaonesha kuwa TICTS walihudumia makontena ya futi 20 (TEUs) 606,169 mwaka 2021 ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.8 tu kulinganisha na mwaka 2020.
TICTS wameshindwa kufikia lengo la kimkataba la kuongeza mzigo wa kontena kwa asilimia 37 kwa mwaka.
Post A Comment: