Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) Neema Mwakalyelye akizungumza na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Ikungi juzi wakati wa ziara yake ya siku moja ya kukagua ujenzi wa Chuo cha Ufundi  ambapo aliipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)-Kanda ya Kati-Dodoma kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa mradi wa Chuo cha Ufundi cha VETA Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.
Msimamizi wa ujenzi wa chuo hicho, Daudi Mrutu (kushoto) akitoa maelezo ya ujenzi wa chuo hicho kwa Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) Neema Mwakalyelye (wa nne kutoka kulia. Wengine kutoka kulia ni Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Widege Mzalendo, Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati Dodoma, John Mwanja na  Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Ikungi, Erick Nyoni.
Ukaguzi wa jengo la Utawala wa chuo hicho ukifanyika.
Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati Dodoma, John Mwanja (wa pili kulia) akitoa maelezowakati wa ukaguzi wa jengo la utawala wa chuo hicho.
Safari ya ukaguzi wa majengo ya chuo hicho yakifanyika.
Muonekano wa moja ya nyumba ya walimu wa chuo hicho.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Widege Mzalendo (kushoto) , akielekeza jambo wakati wa ukaguzi huo.
Muonekano wa baadhi ya majengo ya chuo hicho.
Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) Neema Mwakalyelye (katikati) akiangalia baadhi ya samani zilizonunuliwa kwa ajili ya chuo hicho.
Msimamizi wa ujenzi wa chuo hicho, Daudi Mrutu (kulia) akitoa maelezo wakati akionesha vifaa mbalimbali vilinyonunuliwa kwa ajili ya chuo hicho.
Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) Neema Mwakalyelye akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro wakati wa mkutano wa kupata taarifa ya ujenzi uliofanyika ukumbi wa chakula wa chuo hicho.
Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati Dodoma, John Mwanja akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa chuo hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro akizungumza wakati wa mkutano huo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Singida, Mika Likapakapaaakizungumza katika mkutano huo.. Kushoto ni Katibu wa CCM Wilaya ya Ikungi Stamili Dendego na kulia ni Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Widege Mzalendo.
Mkutano ukiendelea.
Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) Neema Mwakalyelye (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Ikungi. Kutoka kulia waliosimama mbele ni ni Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Ikungi, Erick Nyoni, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida,Widege Mzalendo, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi,Jerry Muro, Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Mika Likapakapa na Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati Dodoma, John Mwanja. Waliosimama nyuma kutoka kushoto ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ikungi (OCD) Suzana Kidiku na kushoto kwake ni Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Winfrida Funto.
 

Na Dotto Mwaibale, Singida

NAIBU Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) Neema Mwakalyelye ameipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)-Kanda ya Kati-Dodoma kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa mradi wa Chuo cha Ufundi cha VETA Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

Mwakalyelye alitoa pongezi hizo juzi wakati akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Ikungi wakiwepo wajumbe wa kamati ya ulizi na usalama wa wilaya hiyo alipokuwa katika ziara ya siku moja ya kutembelea chuo hicho na kukagua ujenzi wake uliofanywa na VETA Kanda ya kati kwa kusimamiwa na TAKUKURU.

Aliwapongeza VETA kwa kukamilisha ujenzi huo kwa muda mfupi na kuwa amefarijika sana na kama wanavyofahamu Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa miradi ya namna hiyo ya kimkakati na akasisitiza kuwa litakuwa ni jambo la kuvunja moyo na kuhuzunisha pale ambapo kutakuwa na ufujaji au upotevu wa utekelezaji wa mradi ambao hauonekani moja kwa moja lakini unaonekana katika viwango vya mradi husika.

“Nifaraja nimekuja na kuona hatua mliyofikia majengo mliyojenga na miundombinu ipo katika viwango tarajiwa vinavyotakiwa na Serikali na hilo nalo ni sababu nyingine ya kuwapongeza wale wote mlioufikisha ujenzi huu katika hatua hii nzuri licha ya mradi kuwa na changamoto kubwa” alisema Mwakalyelye.

Alisema VETA wanakuwa mfano wa kuigwa kwa sababu miradi ya namna hiyo inaendelea katika sehemu mbalimbali ya nchi na kama mkurugenzi alivyosema kuwa nia ya Serikali ni kuwa mwaka wa fedha ujao kila wilaya ambazo ni takribani 62 zitakuwa na miradi yenye sura kama hiyo ikiendelea.

Alisema kutokana na hali hiyo hatarajii kusikia VETA amekwenda Waziri Mkuu kufungua mradi wa chuo na kukutana na sintofahamu  kwa sababu Ikungi wanauzoefu wa kutosha wa kuonesha miradi ya namna hiyo inaweza kufanyika na thamani ya fedha ikaonekana na kupatikana .

“Nimtake Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati Dodoma John Mwanja ampelekee ujumbe huu Mkurugenzi Mkuu wa VETA nchini kuona kwamba miradi kama hii inayofanywa vizuri itumike kama miradi ya mafunzo ya ndani kwa ajili ya kujengeana uwezo katika maeneo mengine ambayo miradi ya namna hiyo inapelekwa” alisema Mwakalyelye..

Alisema haitakuwa na maana kuona mradi wa Ikungi umekamili vema lakini baada ya siku au miezi kadhaa katika maeneo mengine eti mkuu wa chuo au mkurugenzi wa kanda wa VETA wamesimamishwa kwa ujenzi uliochini ya kiwango hivyo kwa uzoefu huo walioupata Ikungi wautumie katika maeneo mengine ili kuepuka hasara inayoweza kutokea kutokana na watu wasio na ufahamu kamili au kuwa na nia ovu ambapo aliomba wapewe ushirikiano katika uendelezaji wa wilaya hiyo ambayo inakuwa kwa kasi kubwa.

Aidha Mwakalyelye aliwataka viongozi wilayani humo kuhakikisha wanasimamia vizuri ununuzi wa mbembejeo za kilimo na mapato yote yanayokusanywa yanaingizwa kwenye akaunti za Serikali na si vinginevyo.

Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati John Mwanja akitoa taarifa ya ujenzi wa chuo hicho alisema Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Ikungi chenye umiliki wa Hati namba: 2218- SGD  kinajengwa  katika  Kijiji  cha Muungano,Kata  ya Unyahati  wilayani  Ikungi  katika  mkoa  wa Singida kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 50.

Alisema Mradi huo  ulianza mnamo mwezi Machi, 2020 ukisimamiwa na chuo cha VETA Singida na ulipaswa kutekelezwa kwa muda wa miezi sita hata hivyo, haukuweza kukamilika kwa wakati kutokana na changamoto kadhaa zilizojitokeza na baadaye mradi kusimama kwa muda wa mwaka mmoja.

Alisema Mkurugenzi Mkuu wa VETA Februari 28/2022 alihamishia majukumu ya usimamizi wa Ujenzi wa chuo hicho  kutoka Chuo cha VETA Singida kwenda ofisi ya  Mkurugenzi wa VETA Kanda ya kati ambaye hadi sasa ndiye anaendelea na usimamizi wa ujenzi huo ambao unatekelezwa kwa  mfumo wa “Force Account”.

Akizungumzia utekelezaji wa ujenzi huo alisema unahusisha jumla ya majengo 17 ambayo ni Jengo moja la utawala, Majengo manne  ya karakana, jengo moja la madarasa mawili makubwa, majengo mawili  ya mabweni  (Wasichana na Wavulana), Bwalo la chakula na Jiko, Majengo Matatu  ya vyoo (Wasichana Wavulana  na  Watumishi),  nyumba  mbili  za  watumishi,  jengo  la  umeme,  Jengo  la  bohari  na kibanda cha mlinzi. Kwa wastani hatua ya ujenzi hadi sasa imefikia asilimia 96.

Mwanja alisema mradi wa ujenzi wa chuo hicho unatarajiwa kukamilika mwishoni katikati ya mwezi Novemba, 2022 na kuwezesha kutoa nafasi ya kufanya ukamilishaji wa taratibu zingine zenye kuwezesha utoaji wa mafunzo katika chuo.

Alisema  chuo kitakapokamilika, kitaendesha mafunzo ya kozi ndefu na fupi na kkuwa ya muda mrefu yatachukua muda wa miaka miwili hadi mitatu ambayo  yatatolewa katika fani zipatazo sita katika awamu ya kwanza mara chuo kitakapokamilika ambazo ni Uhazili na Kompyuta (Secretarial and Computer Application),Ushonaji (Design Sewing and Cloth Technology), Uashi (Masonry and Bricklaying),Umeme wa Majumbani (Electrical Installation),Ufundi Magari (Motor Vehicle Mechanics) na Uchomeleaji Vyuma (Welding and Metal Fabrication).

Alisema chuo  kitakuwa  na  uwezo  wa  kudahili  wanafunzi  240  wa  kozi  ndefu  na  uwezo  wa  kuchukua wanafunzi 144 wa bweni  (wasichana 64 na wavulana 80).

Alisema pia, kutakuwa na mafunzo ya muda mfupi (Short Courses) yatakayochukua muda wa mwezi mmoja hadi miezi sita kwa wastani mafunzo hayo yanakadiriwa kudahili wanafunzi wapatao 250 hadi 900 kwa mwaka kutegemeana na mahitaji ya jamii na shughuli za kiuchumi za eneo hilo.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: