Na. Michael Msombe, Mbeya
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Rais-TAMISEMI imeahidi kuboresha miundombinu ya barabara na elimu kutokana na uwepo wa changamoto hizo katika Jiji hilo.
Hayo yamebainishwa leo Oktoba 5, 2022 na Katibu Mkuu wa TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe wakati akizungumza na Baraza la Madiwani wa Jiji hilo mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi ya kutembelea na kukagua miundombinu ya barabara shule za msingi na sekondari.
Prof. Shemdoe amesema kuwa licha ya Mbeya kuwa Jiji bado lina changamoto nyingi ambazo amejionea na kueleza kwamba Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kufanya maboresho makubwa na ya kihistoria.
Akitolea mifano ya hatua ambazo Serikali imeshakwisha anza kuifanya ndani ya Jiji hilo, amesema kuwa hadi sasa tayari Halmashauri Jiji inaendelea na utekelezaji wa miradi ya elimu yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 2/=.
Prof. Shemdoe amesema katika kutelekeza hayo Serikali imepanga kutangaza zabuni ya kuboresha barabara, kiwanja cha ndege na mifumo ya maji na mwishoni mwa mwezi Oktoba na mwanzoni mwa mwezi Novemba 2022 na kazi rasmi kuanza mwezi Machi 2023.
Baadhi ya miradi aliyoitaja kuanza ni Pamoja na ujenzi wa stendi kuu ya mabasi na stendi ndogo katika eneo la Airport ya zamani, Upanuzi wa barabara ya Iziwa (km 5.75), Upanuzi wa barabara ya block T-Makunguru na Juhudi (km 3.3), Upanuzi wa barabara ya uyole-Itezi (km 2.0), Upanuzi wa barabara ya Airport-Samora-TANESCO-Sae-Kisanji na Kabwe Block T-Sido (km 3.2) Pamoja na uboreshaji na upanuzi wa mifumo ya maji eneo la Nzovwe.
Akishukuru kwa niaba ya Baraza la Madiwani na wananchi wa Jijini Mbeya, Mhe. Dkt. Tulia Ackson ambaye ni Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo hilo, amesema kuwa Jiji la Mbeya linayo Imani kubwa sana na Serikali ya Rais Samia na kuiomba kuliangalia kwa jicho la upekee kutokana na kwamba Jiji hilo limekuwa na hali mbaya katika sekta nyingi kwa muda mrefu.
“Ndugu Katibu mkuu, changamoto zinazohusika na Ofisi yako zipo nyingi lakini kwa hapa kwetu kipaumbele chetu kikubwa ni miundombinu ya barabara na elimu, Kiukweli kabisa hali sio nzuri na uzuri wewe mwenyewe umetembelea baadhi ya maeneo na umejionea hivyo basi tunakuomba ukitoka hapa ulibebe hili kwa uzito mkubwa sana sana” amesisitiza Dkt. Tulia
Post A Comment: