Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kushoto) akizungumza na vijana waliochaguliwa kujiunga kwenye vituo atamizi (hawapo pichani) wakati alipotembelea Chuo cha Mafunzo ya Mifugo (LITA) Kampasi ya Mabuki mkoani Mwanza ambapo amewaeleza vijana hao malengo na matarajio ya serikali ya kuanzisha vituo hivyo, hasa kwa kuhakikisha wanapata ujuzi na uzoefu wa kuweza kufuga mifugo kisasa na kibiashara.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), Dkt. Pius Mwambene (wa pili kulia) akitoa taarifa ya uendeshaji wa vituo atamizi katika Chuo cha Mafunzo ya Mifugo (LITA) Kampasi ya Mabuki na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) - Mabuki mkoani Mwanza kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa tatu kutoka kulia) ambapo amesema tayari baadhi ya vijana wameshafika na wanaendelea na maandalizi.
Mkurugenzi wa Utafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Dkt. Daniel Komwihangilo (wa pili kutoka kushoto) akiwasihi vijana waliochaguliwa kujiunga na vituo atamizi kuhakikisha wanafanya kazi za ufugaji kwa vitendo kwa bidii ili malengo yaliyokusudiwa na serikali dhidi yao yaweze kutimia.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya ufugaji mifugo kisasa na kibiashara wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (hayupo pichani) wakati alipotembelea Chuo cha Mafunzo ya Mifugo (LITA) Kampasi ya Mabuki mkoani Mwanza kukagua kazi zinazoendelea kwa ajili ya uanzishaji vituo atamizi.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene (kulia waliokaa), Mkurugenzi wa Utafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Dkt. Daniel Komwihangilo (kushoto waliokaa) pamoja na watumishi wa LITA na TALIRI Mabuki na vijana waliochaguliwa kujiunga kwenye vituo atamizi mara baada ya Waziri Ndaki kumaliza kuzungumza na vijana hao kwenye Kampasi ya Mabuki mkoani Mwanza.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa nne kutoka kulia) akizungumza na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene (wa pili kutoka kushoto) wakati alipofika kwenye Chuo cha Mafunzo ya Mifugo (LITA) Kampasi ya Mabuki Mkoani Mwanza kukagua kazi zinazoendelea kufanyika kwenye eneo litakalotumika kwa ajili ya vituo atamizi ambapo amewataka viongozi wa LITA kuhakikisha kazi hizo zinakamilika kwa wakati.
.....................................
Programu ya Samia Ufugaji kwa Tija inakwenda kumaliza changamoto ya upatikanaji wa mifugo bora inayohitajika kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki wakati anazungumza na vijana waliochaguliwa kujiunga na vituo atamizi kwa ajili ya kupata mafunzo ya ufugaji kwa vitengo katika Chuo cha Mafunzo ya Mifugo Kampasi ya Mabuki mkoani Mwanza ili waweze kufuga kisasa na kibiashara.
Waziri Ndaki amesema kuwa prograu hii kwanza imelenga kuwabadilisha vijana kifikra kwa kuwapatia mbinu mbalimbali za ufugaji wa kisasa na kibiashara ikiwa ni pamoja na kuwaonyesha fursa zilizopo kupitia Sekta ya Mifugo na namna ya kuzitumia kwa tija.
Programu hii imeanzishwa kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati wa kuhitimisha sherehe za Wakulima – Nanenane zilizohitimishwa mkoani Mbeya ambapo aliagiza Sekta ya Mifugo kuanzisha vituo kwa ajili ya kuwajengea uwezo vijana ili waweze kujiajiri kupitia ufugaji.
Waziri Ndaki amesema kuwa lengo la SAUTI Programu ni kuwawezesha vijana kuanzisha na kuendesha miradi ya ufugaji wa mifugo kibiashara, kuwapatia vijana stadi rahisi kwa vitendo za namna bora ya kuanzisha na kuwekeza katika miradi ya ufugaji wa mifugo, kuwawezesha vijana kupata ujuzi, uzoefu na ujasiri wa kuanzisha miradi ya ufugaji kibiashara, pia kuwaunganisha vijana kwenye mnyororo wa thamani wa uzalishaji wa mazao ya mifugo kibiashara.
Kutokana na malengo hayo, SAUTI Programu inakwenda kuongeza ajira kwa vijana kupitia Sekta ya Mifugo na hivyo kuifanya Sekta hiyo kuongeza kipato kwa wafugaji wenyewe lakini pia mchango wa Sekta kwenye pato la Taifa.
Hivyo amewataka vijana hao kutumia fursa hiyo vizuri kwa kuwa Wizara imeshawaandalia maeneo ambayo watapatiwa mara baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo ili waweze kuanza kufuga kutokana na elimu watakayokuwa wameipata. Pia amewataka vijana ambao wamechaguliwa lakini hawajafika kufika, kwani wasipofanya hivyo watachukuliwa vijana wa akiba kuja kuziba nafasi zilizo wazi.
Aidha, Waziri Ndaki ameendelea kuwasihi viongozi wa mikoa na wilaya kuendelea kusimamia zoezi la uwekaji alama za utambuzi kwenye mifugo katika maeneo yao kwani serikali imeongeza mwezi mmoja ambapo baada ya Oktoba 30, 2022 hatua za kisheria zitaanza kuchukuliwa kwa wafugaji ambao mifugo yao haina alama za utambuzi.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), Dkt. Pius Mwambene amesema kuwa tayari umeshaandaliwa mwongozo utakaotumika kufuga kisasa ambao utawasaidia vijana kama rejea yao hasa pale kutakapokuwa na kitu kinachotaka kuwakwamisha.
Dkt. Mwambene amasema kuwa vijana hao wataanza kujifunza kwa vitendo kuanzia kwenye ujenzi wa mabanda, manunuzi ya chakula na ng’ombe na katika kufanya biashara ili shughuli zote wazielewe.
Mkurugenzi wa Utafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Dkt. Daniel Komwihangilo akiwasihi vijana waliochaguliwa kujiunga na vituo atamizi kuhakikisha wanafanya kazi za ufugaji kwa vitendo kwa bidii ili malengo yaliyokusudiwa na serikali dhidi yao yaweze kutimia.
Akizungumza kwa niaba ya vijana hao, Adelina Bilembo amesema ameishukuru serikali kwa kuanzisha vituo hivyo vyenye lengo la kuwajengea kuwe wa ufugaji kwa vitendo na kuona vijana katika sekta ya mifugo wanahitaji kuwezeshwa. Naye Baraka Ezekiel ameahidi kuwa wataweka juhudi kubwa katika kujifunza ili malengo yaliyowekwa na serikali ya kuwajengea uwezo vijana kupitia ufugaji ifanikiwe na matunda yake yaonekane.
Post A Comment: