Picha ya pamoja baada yakusainiwa kwa mktaba huo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Mkoa Singida, Peter Serukamba, amesema
suala la kushughulikia lishe bora kwa jamii ili kuzuia vifo vya wajawazito na
watoto wanaowaleta hapa duniani ni la kufa na kupona ambapo amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa
Halmashauri kulipa kipaumbele cha kwanza.
Serukamba alitoa agizo hilo jana wakati
akitiliana saini mkataba na ma-DC na ma- DED ikiwa ni agizo lililotolewa na
rais Samia Suluhu Hassan alipokutana na Wakuu wa Mikoa jijini Dodoma
ambapo aliwaagiza kujipanga na kuongeza
jitihada za kuhamasisha utekelezaji wa shughuli za lishe bora.
"Jambo la lishe na afua za lishe ni la kufa
na kupona tulipe kipaumbele cha
kwanza,tukifanikiwa kuifanya jamii yetu iwe na lishe bora hasa kwa watoto
kuanzia umri wa mwaka mmoja hadi mitano tutakuwa tumeweka jiwe msingi kwenye
kizazi kijacho," alisema.
Serukamba alisema madhala ya watoto kukua bila
lishe ni makubwa zaidi kwa jamii ni vile tu hayaonekani haraka hivyo ni jukumu
kwa waganga Wakuu wa Wilaya na wataalamu wanaohusika na lishe kuongeza juhudi
kutoa elimu kwa wananchi wafahamu mpangilio wa vyakula.
"Tunaweza tukawa tunajiuliza kwanini
mitihani watu wanafeli sana tukadhani walimu hawafundishi lakini inaweza kuwa
sababu mojawapo ni madhala ya kutopata lishe bora tena hasa kutoka kwa mama
anapopata mimba," alisema.
Alisema rais Samia ndio 'champion' wa jambo hili
hivyo njia bora ya kumshukru ni kuhakikisha tunamaliza tatizo la lishe ili
kuzuia vifo vya akina mama wajawazito na watoto.
"Unaweza kukuta mtu nyumbani kwake ana kila
kitu lakini anajua matunda ni kwa ajili ya kuuza tu sio kula,akikamua maziwa ni
kuuza tu so kunywa, viongozi wa lishe wa Wilaya tusiishie kwenye makaratasi tu
tuelimishe wananchi wajue mpangilio wa vyakula," alisema.
Mkuu wa Mkoa alisema Wakuu wa Wilaya wahakikishe
wanasimamia suala la lishe ili Mkoa wa Singida utoke kwenye asilimia 87 na
badala yake ufikie asilimia 100.
Serukamba alisema katika kipindi kifupi ambacho
amekuwa katika Mkoa wa Singida amejifunza kuwa watendaji kwenye halmashauri
wanajua kazi sana lakini tatizo lao usipowafuatilia hawafanyi sio kwa makusudi
lakini ndio wameubwa hivyo wanasubiri hadi wasukumwe.
Akiwasilisha Mpango huo wa Afua za Lishe, Kaimu
Afisa Lishe Mkoa wa Singida, Christoweru Barnabas alisema malengo ya mpango huo
ni kuhakikisha wilaya zote
zinasimamia ipasavyo utekelezaji wa afua
za lishe.
Akizungumzia malengo ya mkataba huo alisema Lengo kubwa ni
kufanikisha suala la kuboresha hali ya lishe na kupunguza athari za utapiamlo
katika wilaya,kuhakikisha kuwa
Wilaya inasimamia ipasavyo utekelezaji wa
afua zalishe na kuchukua hatua madhubuti za kupunguza hali duni ya lishe
katika wilaya.
Alitaja malengo mengine kuwa ni kupanga, kutenga na kutoa fedha zote kwa ajili ya kutekeleza afua za lishe katika mipango ya halmashauri kwa mujibu wa miongozo na maelekezo ya Serikali sanjari na kutoa taarifa ya utekelezaji kila mwezi na kila robo mwaka kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa.
Post A Comment: