Na John Walter-
Manyara
Mkuu wa mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere amesema serikali itaendelea kushirikiana na watu wenye ulemavu katika kuwapatia huduma zote zinazohitajika kama watu wengine.
Amezungumza hayo katika kongamano la watu wasioona linalofanyika katika ukumbi wa chuo kikuu huria mjini Babati leo oktoba 19,2022 ikiwa ni maadhimisho ya fimbo nyeupe duniani ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Manyara.
Amesema kongamano hilo ni muhimu kwa watu wasioona kwa kuwa linatoa fursa kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuzifanyia kazi.
Maadhimisho hayo ya fimbo nyeupe yanahusisha Tanzania bara na visiwani.
Kilele cha maadhimisho hayo ni Oktoba 21,2022 na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa yenye Kauli mbiu isemayo “Watu wasioona,tujumuishwe katika ajira,michezo na Teknolojia ya habari na mawasiliano kwa maendeleo endelevu”.
Makamu mwenyekiti wa chama cha wasioona (TLB) Selemani Idrisa amesema mwalimu Julius Kambarage Nyerere ameacha alama kubwa katika nchi kwa watu wasioona ambapo aliwahi kuwapa fursa ya kugusana nae japo hawaoni.
Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi mkoa wa Manyara Simon Lulu amesema chama cha Mapinduzi kitaendelea kuwaunga mkono watu wenye ulemavu katika kila Nyanja kama walivyofanya waasisi wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Karume.
Post A Comment: