Na Gift Mongi Moshi
Miradi mbalimbali ya kimaendeleo iliyoainishwa katika ilani ya uchaguzi ya CCM(2020-2025)katika jimbo la Moshi Vijijini ipo katika hatua mbali mbali za utekelezaji na kuwa itakuwa na mchango mkubwa wa maendeleo pindi itakapokamilika.
Mbunge wa jimbo hilo Prof Patrick Ndakidemi katika ziara yake aliyoifanya jimboni humo amefanikiwa kutembelea
Kata ya Uru Mashariki na kuzungumza na viongozi wa chama cha Mapinduzi wa kata hiyo.
Awali akizungumza na viongozi hao kwa lengo la kupata taarifa za utekelezaji wa ilani unavyoendelea ameeelezwa kuwa kero kubwa zinazowasumbua ni pamoja na kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama katika kata ya Uru Mashariki na ubovu wa barabara za ndani hasa zile za Mwasi Kusini - Mwasi Kaskazini - Mruwia hadi Materuni.
Kero nyingine zilizoainishwa na viongozi hao kwa mbunge huyo ni ile barabara ya Joint Venture na sintofahamu katika ushirika wa Uru East na Mruwia AMCOS ambapo kwa sasa bado dhana ya ushirika inaonekana kusuasua.
Viongozi hao wa chama wamemweleza ndoto yao ya kuona mifereji ya asili ikikarabatiwa ili iwapatie wananchi maji ya kumwagilia kahawa na migomba lakini pia kuweza kufanya kilimo cha mbogamboga.
Hali kadhalika katika mazungumzo hayo yaliyokuwa na dhana ya kujenga maendeleo endelevu swala la uchakavu mkubwa wa shule za msingi Kishumundu na Mnini lilijitokeza.
Kabla ya kuhitimisha ziara yake, Prof Ndakidemi akiwa na viongozi wa chama wa kata, ametembelea jengo la UWT ambalo limechakaa na linahitaji kukarabatiwa kwa kiwango kikubwa.
Tayari viongozi hao wameshafanya jitihada kuhakikisha jengo hilo linajengwa upya ambapo wamemweleza mbunge kuwa mtaalamu anaanda mchoro wa kuboresha jengo hilo na gharama zinazohitajika.
Katika hatua nyingine Prof Ndakidemi akiongozana na diwani wa kata hiyo Samwel Materu na diwani wa viti Maalumu Mh Delina Temba, wamekagua ujenzi wa barabara ya Uru - Mamboleo - Materuni inayokarabatiwa kwa kiwango cha Lami na Moram.
Pia wametembelea madaraja mabovu ya barabara za Kishumundu - Kyaseni, na ile ya Kishumundu - Mwasi Kaskazini ambayo yanaendelea kuporomoshwa na mmomonyoko wa udongo unaotokana na mvua.
Viongozi hawa kwa pamoja wamekubaliana kusaidiana na kushirikiana kwenye ukarabati wa ofisi ya UWT pindi wakati utakapowadia.
Viongozi hao kwa pamoja wamejadiliana na kukubaliana kubeba kero zilizojitokeza kama ile ya kukosekana kwa maji safi na salama na kuazimia kuziwasilisha MUWSA.
Kero za ubovu wa barabara na madaraja wameafikiana kuzipeleka TARURA, na ya uchakavu wa madarasa waliafiki madiwani wazipeleke Halmashauri lakini pia kuhusu swala la joint Venture na sintofahamu katika ushirika wa Uru East na Mruwia AMCOS, mbunge ameahidi kulifikisha katika Kurugenzi ya taifa ya ushirika kwa hatua zaidi.
Katika kufanikisha hayo yote Prof Ndakidemi amewashauri viongozi wahusishe wadau mbalimbali na wananchi katika kujiletea maendeleo badala ya kuisubiri serikali ifanye kila jambo.
Post A Comment: