Timoth Philipo, askari polisi wilayani Busega amefariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa Mkoa wa Simiyu baada ya gari alilokuwa akiendesha kugongana na gari lililokuwa likiendeshwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Blasius Chatanda.

Taarifa iliyotolewa na kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Shadrack Masija leo Jumatano Oktoba 5, 2022  inaeleza kuwa ajali hiyo ilitokea Oktoba 2, 2022 eneo la Mizani Nyakabindi ikimhusisha Chatanda na Philipo.

"Toyota Harrier ilikuwa ikiendeshwa na ACP Chatanda iligongwa na Toyota Mark II ikitokea Bariadi kwenda Lamadi ikiendeshwa na Philipo na kusababisha majeraha kwa madereva wote wawili pamoja na H. 7123 Pc Emmanuel ambaye ni msaidizi wa Chatanda," amesema.


Amebainisha kuwa majeruhi wote walifikishwa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Simiyu kwa ajili ya matibabu na kubainisha kuwa chanzo cha ajali ni uzembe wa Philipo ambaye alihama upande na kwenda upande wa kulia na kisha kuligonga gari liliokuwa likiendeshwa na Chatanda.

Amesema Philipo alifariki dunia Oktoba 3, 2022 akiwa anapatiwa matibabu ikielezwa kuwa sukari ilishuka.

Katika taarifa hiyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limetoa  pole kwa ndugu na familia ya marehemu na taratibu za mazishi zinafanyika kwa kushirikiana na familia na mwili  utasafirishwa kwenda Wilaya ya Magu Mkoa wa Mwanza kwa ajili ya mazishi.

Share To:

Post A Comment: