Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Kazi,Uchumi na Uwekezaji Zanzibar , Dkt Islam Seif Salimu ameipongeza OSHA kwa hatua kubwa inazoendelea kufanya za kulinda nguvu kazi kwa kuhakikisha inaweka mifumo Madhubuti ya usalama na afya katika maeneo mbalimbali ya kazi nchini.
Dkt, Seif amesema hayo jijini Dar es salaam baada ya Watendaji waandamizi kutoka Idara ya Usalama na Afya Zanzibar kufanya Ziara Ofisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahali Kazi (OSHA) kwa lengo la kujifunza namna taasisi hio inavyosimamia sheria ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi
“Kimsingi OSHA imepiga hatua kubwa sana katika usimamizi wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi kwa nchi za Afrika Mashariki hivyo niwapongeze sana kwa kuweka mifumo madhubuti katika usimamizi wa masuala mbalimbali ya usalama na afya kazini hivyo tumeona kuna haja kubwa ya kuja katika taasisi hii kujifunza na kushirikiana nao katika masuala mbalimbali ikiwemo kutengeneza mkakati wa pamoja wa kuhakikisha maeneo yetu ya kazi yanakuwa salama” alisema Dkt, Islam Seif Salim
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi.Khadija Mwenda amesema kuwa taasisi yake itaendelea kuimarisha ushirikiano na Idara ya Usalama na Afya ya Zanzibar ili kujenga ustawi wa wafanyakazi wote nchini.
“Tumekuwa na ushirikiano mzuri sana na wenzetu wa Wazanzibar katika mambo mbalimbali kiwemo usimamizi wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi, ziara hii imejikita zaidi katika kujifunza namna tulivyofanikiwa kutoka katika kitengo ndani ya idara ya kazi mpaka kujitengemea kama wakala na tunaamini kuwa itawapa chachu ya kufanya mapinduzi juu ya uboreshaji wa masuala ya usalama na afya katika maeneo ya kazi” alisema Mtendaji Mkuu, Bi Khadija Mwenda akiongeza kuwa.
“Tumeshuhudia Zanzibar ikikua kiuchumi kwa haraka sana na shughuli nyingi za kiuchumi zinapofanyika zinakuja na vihatarishi ambavyo vinahitaji mbinu mbadala ya kukabiliana navyo na ndio maana wamekuja kujifunza ni namna gani sisi tumeweza kufanya usimamizi lakini zaidi tutakuwa na ushirikiano mzuri katika usimamizi wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi ili kujenga ustawi wa wafanyakazi wote Nchini”
Aidha Mkurugenzi wa Idara ya OSH Zanzibar, Dkt. Ali Said Nyanga amesema kuwa kupitia ziara hii itawasaidia kutatua changamoto mbalimbali walizokuwa wakikumbana nazo wakati wakitoa huduma vilevile itawasaidia kulinda nguvu kazi kwa kuhakikisha mazingira yote ya kazi yanakuwa salama.
“Tumekuwa tukikumbana na changamoto mbalimbali katika utoaji huduma na changamoto hizo zimepatiwa majibu mahali hapa pia tumeshuhudia ongezeko kubwa sana la uwekezaji nchini ambao utahitaji sana huduma zetu hivyo nilazima tuhakikishe nguvu kazi hizi zinalindwa ipasavyo iliziweze kuzalisha mara dufu” alisema Mkurungezi wa Idara ya Usalama na Afya kazini, Dkt. Ali Said Nyanga.
Idara ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi nchini Zanzibar ni idara iliyo chini ya Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji yenye jukumu la Kusiamia masuala ya usalama na afya katika maeneo ya kazi Tanzania Visiwani (Zanzibar).
Post A Comment: