Naibu Waziri wa Kilimo Mh. Anthony Mavunde amezitaka Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Kilimo kuhakikisha zinayapima maeneo yao ili kupata hati za umiliki wa ardhi na pia kuweka uzio katika maeneo yote ili kupunguza migogoro isiyo ya lazima na kupunguza uvamizi wa maeneo hayo.
Naibu Waziri Mavunde ameyasema leo mkoani Mwanza wakati wa kikao cha utatuzi wa migogoro ya ardhi ya Vijiji 975 inayoshughulikiwa kamati ya Mawaziri nane wa kisekta ambapo leo kamati hiyo ilikuwa katika Kata ya Shibula,Wilaya ya Ilemela-Mwanza.
“Ni wakati muafaka sasa Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya kilimo kuhakikisha mnayalinda na kuyatunza maeneo yenu kwa kuyapima na kuzungushia uzio.
Kuyaacha mashamba haya bila kuyatumia kwa eneo kubwa kunasabisha uvamizi wa maeneo haya ambayo mengi yametengwa kwa ajili ya uzalishaji mbegu na utafiti wa kilimo.
Hivyo naagiza Taasisi zote kuhakikisha mnatenga bajeti ya kulinda haya maeneo na kusimamia malengo ya matumizi yake,Mh.Rais Samia Suluhu Hassan ametuongezea bajeti kwenye wizara yetu hivyo hakikisheni katika mipango yenu inahusisha ulinzi wa maeneo haya”Alisema Mavunde
Katika zoezi hili jumla ya hekta 92 zilizopo katika eneo la Taasisi ya Utafiti ya Kilimo Ukiriguru zimegawiwa kwa wananchi ili kuruhusu shughuli za kilimo zinazofanywa na wananchi katika eneo hilo kama njia ya utatuzi wa mgogoro huo.
Post A Comment: