Siku chache baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana kutoa taarifa moto uliokuwa umewaka Mlima Kilimanjaro umedhibitiwa, moto huo umelipuka tena katika maeneo ambayo awali yalidhibitiwa kutokana na upepo mkali.
Moto huo ulinza kuwaka Oktoba 21, 2022 katika eneo la Karanga kuelekea Baranco mita 3,963 kutoka usawa wa bahari ambapo mpaka sasa hakuna madhara yoyote ya kibinadamu yaliyojitokeza na shughuli za utalii zinaendelea kama kawaida.
Mpaka sasa vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na wadau wa utalii viko katika maeneo hayo kukabiliana na moto huo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Oktoba 25, 2022, Katibu mkuu wa hizo, Profesa Eliamani Sedoyeka amesema watu zaidi ya 400 wapo katika maeneo hayo kukabiliana na moto huo ambao umetokana na upepo mkali uliopo kwa sasa.
"Jana usiku ilitokea mioto mitatu tofauti na leo asubuhi timu za watu mbalimbali waliondoka kwenda kukabiliana na moto huo na hadi kufika saa saba tumefanikiwa kuuzima moto mmoja na kubakia mioto miwili na timu zimeendelea kupambana ili kuweza kuuzima," amesema
Aidha amesema mpaka kufikia saa 10 jioni kumekuwa na mafanikio makubwa katika kukabiliana na moto huo kama hali ya hewa haitabadilika, wataweza kuukabili.
Post A Comment: