WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ameruhusu Magari kuanza kutumia daraja jipya la wami kufuatia Ujenzi wake kukamilika.

Profesa Mbarawa amewataka viongozi na wananchi wa mkoa wa Pwani, Kuhakikisha daraja hilo linalindwa ili kudumu kwa zaidi ya miaka 120 iliyokusudiwa kutumika.

"daraja limekamilika kwa asilimia 96 hivyo madereva na watumiaji wa daraja hili, tumieni kwa uangalifu na kulitunza kwa kuwa kazi ndogo ndogo za ukamilishaji zikiendelea." amesema Prof.Mbarawa.

Aidha, Prof. Mbarawa amewataka viongozi kutoa ushirikiano kwa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na wakandarasi wanaojenga barabara ya magari yaendayo haraka ya Kibaha-Chalinze-Morogoro Express Way (km 215)Ili kuwezesha Ujenzi kuanza kwa wakati.

"Serikali inaendelea kuufungua mkoa wa Pwani kwa kuendeleza Ujenzi wa barabara kutoka Pangani-Horohoro-Lungalunga- hadi Mombasa nchini Kenya ambayo itaboresha uchumi wa viwanda na kukuza utalii katika eneo hilo la kimkakati," ameongezea Profesa Mbarawa.

Kwa Upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Eng. Dorothy Mtenga, amesema zaidi ya shilingi bilioni 75 zimetumika katika Ujenzi wa daraja hilo lilokusudiwa kutatua changamoto za daraja la mwanzo ambalo lilikuwa halikidhi mahitaji ya magari yanayopita kwa kuwa lilijengwa miaka 63 iliyopita na lilikuwa na njia moja.

Naye Mkuu wa Wiaya ya Bagamoyo, Bi Zainabu Abdalah Issa, ameishukuru Serikali hususani Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa utekeleza wa miradi ya miundombinu ya kimkakati katika Mkoa wa Pwani, inayochochea maendeleo ya Viwanda, Utalii na Biashara.

Aidha, amemhakikishia Waziri Mbarawa, kuwa madaraja na barabara zinazojengwa katika mkoa wa Pwani, zitatunzwa vizuri.

Kwa upande wake Mbunge wa Chalinze ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Ridhiwani Kikwete, ameishukuru Serikali kwa kuendeleza miradi ya miundombinu katika mkoa wa Pwani ili kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo.

Daraja jipya la Wami, lenye urefu wa mita 513.5, upana mita 11.85 na barabara unganishi km 3.8 linaunganisha mkoa wa Pwani na Tanga, litachochea ustawi wa jamii kiuchumi na kuleta maendeleo kwa mikoa ya kaskazini mwa Tanzania.



Share To:

Post A Comment: