Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile amefunga rasmi mashindano ya Ligi la Daraja la Nne Wilaya ya Kondoa, ambapo amegawa jezi za mpira wa miguu seti nane na Sh Milioni Moja kwa Timu nane ambazo zimefuzu kucheza hatua ya nane bora ya Ligi hiyo.

Akizungumza mara baada ya kugawa zawadi kwa washindi wa Ligi hiyo ambayo imemalizika katika vituo vitatu vilivyokua vimepangwa, Mbunge Ditopile ameahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwemo michezo, elimu, afya, maji na kiuchumi.

Ditopile amesema yeye kama Mbunge anathamini juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kuendeleza sekta ya michezo kwani anatambua namna ambavyo michezo imekua ajira muhimu kwa vijana nchini.

" Ninathamini na kutambua kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia katika kuendeleza michezo nchini ndio maana nimeona nichangie kiasi hiki cha Sh Milioni Moja kwa washindi na jezi seti nane kwa washindi nane wa vituo vitatu ambavyo mashindano haya yalichezwa"

"Lengo langu kama Kiongozi wenu ni kuona Wilaya yetu ya Kondoa inazalisha vijana wengi katika kiwanda cha michezo haswa kwenye Soka kwa kuwezesha miundombinu rafiki ikiwemo viwanja vya michezo, vifaa vya mazoezi na zaidi kuwezesha mafunzo kwa waamuzi wetu ili kukuza michezo Wilayani kwetu"

"Nafahamu kuna hatua ya nane bora inakuja, niwaahidi Ofisi yangu iko wazi muda wote kuhakikisha michuano hii inafanyika kwa kuwezesha upatikanaji wa zawadi kwa washindi wote lakini zaidi mafunzo kwa waamuzi wetu ili kuongeza weledi katika kusimamia sheria 17 za Soka."

Ditopile amewaomba Wananchi wa Kondoa kuunga mkono juhudi za Chama cha Soka Wilaya ya Kondoa katika kukuza mchezo huo huku akitoa rai kwa viongozi wa vyama vingine vya michezo wilaya ya Kondoa kuandaa mashindano ambayo yataibua na kukuza vipaji vya vijana ili kuwa na idadi kubwa ya vijana kwenye kiwanda cha michezo.

" Lengo letu ni kuona Wilaya ya Kondoa inazalisha akina Samatta na Msuva wengi kwenye Soka, kuzalisha vijana wengi wenye vipaji kama wale Ramadhan Brothers walioshinda shindano la Australia Got Talent, kwa pamoja tukiungana tunaweza kuifanya Kondoa yenye vipaji vikubwa ndani na nje ya Nchi yetu," Amesema Mbunge Ditopile.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa KDFA, Msekela Majuto amemshukuru Mbunge Ditopile kwa kukiunga mkono Chama hicho katika jitihada za kuinua vipaji vya vijana wa Wilaya hiyo huku akiahidi kuendelea kuboresha mashindano hayo Ili yazidi kuwa bora siku hadi siku.



Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: