Mgeni rasmi wa kilele cha maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima nchini, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Juma Kipanga amefurahia kuona wanufaika wa Mafunzo ya Kuendeleza Ujuzi yanayofadhiliwa na Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) na kusimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) wanaweza kutumia mafunzo hayo katika kujipatia kipato.
Mhe. Kipanga amesema hayo alipotembelea banda la maonesho la TEA katika kilele cha maadhimisho na maonesho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima yanayoendelea kwenye viwanja vya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) Jijini Dar es Salaam. Juma hilo lilianza tarehe 17-21 Oktoba 2022.
Akiwa bandani hapo Mhe. Kipanga alizungumza na wanufaika wa mafunzo ya Kuendeleza Ujuzi (SDF), Esther Shebe ambaye ni mkulima wa Uyoga jijini Dar es Salaam pamoja na Azalia Madege ambaye alipata mafunzo ya kuendesha na kutengeneza pikipiki za miguu miwili na mitatu na kwasasa ameajiriwa katika kampuni ya kuagiza na kuuza pikipiki ya Fekon kama fundi.
Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) ni sehemu ya Programu ya Kuendeleza Elimu ya Ujuzi na Mafunzo ya Stadi za Kazi zenye kuleta Tija katika Ajira (ESPJ) na Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza na Kuendeleza ujuzi nchini (NSDS) ambayo inasimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na inafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Benki ya Dunia (WB)
Zaidi ya wananchi 36,870 wamenufaika na ruzuku ya Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi ili kuwawezesha kuajiriwa au kujiajiri wenyewe. Awamu ya kwanza ya SDF ilianza kutekelezwa mwaka wa fedha 2018/2019 ambapo Taasisi 15 zilifadhiliwa kwa jumla ya Shilingi Bilioni 3.1 wakati katika awamu ya pili Taasisi 81 zimenufaika kwa ufadhili wa kiasi cha Shilingi Bilioni 9.7 zikitumika kuendesha programu za mafunzo ya ujuzi.
Post A Comment: