Kwa mujibu wa Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Morogoro, Elizeus Rwegasira, Jeshi la Polisi limekuwa likiwazuia kufanya shughuli za kisiasa bila sababu za msingi.
Alisema jana kuwa kwa nyakati tofauti chama hicho wilayani huko kimekuwa kikiandaa shughuli za kisiasa, lakini kinapotoa taarifa kwa jeshi hilo, kuhusu shughuli hizo huzuiliwa kwa kutoa sababu mbalimbali.
Rwegasira alitoa mfano kuwa Septemba 31 mwaka huu, waliandaa mkutano na kuandika barua kwenda kwa jeshi hilo kuomba ulinzi wa mkutano wa hadhara waliokuwa wamepanga kuufanya katika viwanja vya Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, wakazuiwa kwa madai kuwapo shughuli za Sensa ya Watu na Makazi.
Alisema tukio la hivi karibuni ni la kuzuiwa kwa msafara wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika kupita Msamvu alipoalikwa kwenda kufungua mafunzo ya vijana wa chama hicho.
“CHADEMA Wilaya ya Morogoro Mjini kiliandaa mafunzo kwa vijana Oktoba 16 mwaka huu kwa ajili ya kuwezesha usajili wa wanachama kidijitali na kilimwalika Mnyika kuwa mgeni rasmi lakini polisi walimzuia.
“Kwa kuwa Katibu Mkuu aliandaliwa mapokezi pindi anapofika mjini Morogoro, mimi (Rwegasira) nilikwenda Ofisi ya Kamanda wa Polisi Wilaya ya Morogoro Mjini, Oktoba 14 mwaka huu kumpatia taarifa ya ujio huo ili kuondoa uwezekano wa polisi kuingilia mapokezi hayo na kusababisha vurugu.
“Kamanda alinieleza kuwa siku hiyo wakubwa wao watakuwa na semina karibu na eneo ambalo tulikuwa tumepanga kupita na msafara baada ya kumpokea Katibu Mkuu wetu, hivyo ingeleta taswira isiyo nzuri machoni mwa wakubwa hao.
"Kwa hiyo, walituzuia tusipite katika barabara hiyo na kutupangia eneo lingine, kitendo ambacho kilitupotezea muda na kuzua taharuki isiyo ya lazima," alidai.
Alilitaka Jeshi la Polisi Wilaya ya Morogoro kuzingatia weledi katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na katiba, ikiwamo kutoa huduma bila ubaguzi na kuacha kutumia nguvu.
“Ndio maana tunahitaji Katiba Mpya ili kuondoa mkwamo wa jeshi kuendelea kutumia taratibu za kikoloni kutimiza majukumu yake,” alisema Rwegasira.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro kuzungumzia suala hilo, simu ilipokewa na msaidizi wake aliyedai alikuwa kwenye kikao.
Post A Comment: