Na John Walter-Hanang
Bodi ya maji bonde la kati (IDBWB) imezindua jumuiya mbili za watumiaji maji Ziwa Bassotu na bonde dogo la Endagaw zilizopo wilaya ya Hanang mkoani Manyara na kufanya idadi ya mabonde katika kanda hiyo kufika tisa.
Mkurugenzi wa Bodi ya maji Bonde la Kati Damford Samson ameeleza ni Muhimu kuhifadhi vyanzo vya Maji kwa vizazi vya sasa na vijavyo kwani vikiharibiwa maji yatatoweka na viumbe hai vyote akiwemo binadamu.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa jumuiya hizo leo Oktoba 13,2022, amesema wizara ya maji imeamua kuziunda Jumuiya hizo ili zikawe chachu katika kutunza vyanzo vya Maji kwa kukumbushana kuacha kufanya Shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kama inavyoelekeza Sheria namba 20 ya mwaka 2014 kuepuka uharibu.
Mkuu wa wilaya ya Hanang' Janeth Mayanja akizungumza katika halfa hiyo, amesema Ziwa Bassotu limepoteza uhalisia wake kutokana na uharibu uliofanywa na Wananchi kwa kufanya Kilimo pembezoni mwa ziwa na shughuli zingine.
Mayanja amesema Maji hayana mbadala hivyo Jumuiya ziendelee kuwa imara katika maeneo yao na kusimamia kama miongozo yao inavyoelekeza.
“Maji hayana mipaka ya kiutawala yeyote anaweza kutumia popote”.
Ameagiza jeshi la polisi kutoa ushirikiano kwa Jumuiya hizo pindi zinaporipoti uharibu kwenye vyanzo vya Maji ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Ameiomba Bodi ya Bonde la Kati kusaidia kubaini chanzo cha maji Endasak na mipaka yake ili kuondoa migogoro kwa Wananchi wanaotumia maji hayo.
Aidha Jumuiya hizo zilizozinduliwa leo zimekabidhiwa vitendea kazi zikiwemo katiba na vitambulisho vyenye majina yao.
Jumuiya hizo za watumia maji Ziwa Bassotu na bonde dogo la Endagaw zimeahaidi kusimamia vyema jumuiya zao na kulinda vyanzo vya maji kwa maendeleo endelevu.
Kauli mbiu inayoongoza Jumuiya hizo inasema “Utunzaji wa vyanzo vya maji ni jukumu letu sote”
Post A Comment: