SERIKALI imeidhinisha kiasi cha Sh bilioni 59.58 cha ruzuku ya mafuta kwa mwezi Oktoba ambapo sasa bei ya lita ya petroli itapungua kwa Sh 133 kwa Dar es Salaam, Sh 204 kwa Tanga na Sh 118 kwa mafuta yanayopakuliwa kupitia bandari ya Mtwara.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) inachapisha bei elekezi ya bidhaa za petroli, zinazotumika Tanzania Bara kuanzia kesho, Oktoba 5 ambapo bei ya rejareja itakuwa Sh 2,886 kwa lita ya petroli, Sh 3,083 kwa lita ya dizeli na Sh 3,375 kwa mafuta ya taa kwa Dar es Salaam.

Kwa mafuta yanayo pakuliwa Tanga, lita ya petroli itauzwa kwa Sh 2,924 mafuta ya dizeli Sh 3108 na mafuta ya taa Sh 3,275. Vilevie bei ya lita ya mafuta ya petroli kwa Mtwara itakuwa Sh 2,908 na dizeli itauzwa kwa Sh 3,099.

Gharama ya dizeli imepungua kwa Sh 275 kwa Dar es Salaam, Sh 360 kwa Tanga na Sh 333 kwa Mtwara.

EWURA imesema bei za mafuta katika soko la dunia zimepungua bei kwa kuzingatia kikikotoo kilichotumika mwezi Agosti ambapo petroli imepungua kwa asilimia 7.4, dizeli asilimia 3.9 na mafuta ya taa asilimia 1.9.

Hata hivyo, EWURA imesema athari za upungufu huo zimezidiwa na ongezeko la malipo ya Premium katika soko ambalo limepanda kwa kati ya asilimia 50 na asilimia 163 kulingana na bandari.

EWURA imesema dhamira ya serikali kutoa ruzuku ya Sh bilioni 59.58 kwa mwezi Oktoba zimesaidia kupunguza athari mbaya za bei ya juu ya mafuta kwa umma na uchumi kwa ujumla.

Bei ya Mafuta kuanzia Oktoba 5| Ewura


Share To:

Post A Comment: