Waziri Jenister Mhagama katika moja ya hafla ya kuhamasisha matumizi ya Lishe bora kwa watoto |
Lishe ina uhusiano na afya ya akili_ hivyo mtoto anahitaji lishe kamili ili kuwa na afya njema pamoja na akili timamu. |
Na Abby Nkungu, Singida
ASILIMIA 97 ya watoto wenye umri chini ya miaka miwili mkoani Singida
hawapati mlo kamili unaokubalika na waatalamu wa lishe bora, hali inayochangia
kupata changamoto mbalimbali za kiafya; ikiwemo udumavu, ukondefu na uzito
mdogo.
Taarifa ya Utafiti wa Kitaifa wa Lishe (TNNS) uliofanyika mwaka 2018, inaonesha kuwa ni asilimia tatu tu (3%)
ya watoto wenye umri wa chini ya miaka miwili mkoani Singida ndio wanaopata mlo
unaokubalika kilishe.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Victorina
Ludovick ilieleza kuwa lishe duni ni moja
ya sababu zinazochangia kuendelea kuwepo kwa tatizo la udumavu mkoani
humo kwa asilimia 29.8, ukondefu asilimia 4.7 na uzito pungufu asilimia 14 kwa watoto walio chini ya miaka mitano.
Hata hivyo, alisema kuwa pamoja na hali kuwa bado sio ya kuridhisha,
matatizo hayo yamepungua ikilinganishwa na miaka minne kabla ya kutafiti huo
(yaani 2014) ambapo udumavu ulikuwa
asilimia 34, ukondefu asilimia 5 na
uzito mdogo asilimia 15.
“Maendeleo sio mabaya. Hii Programu Jumuishi ya Taifa ya miaka mitano juu
ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto itasaidia kuleta matokeo
chanya zaidi katika suala la lishe kwani inahusisha masuala mtambuka” alisema
na kuongeza kuwa ni suala la muda tu kumaliza changamoto hiyo.
Alieleza kuwa chini ya Programu hiyo, wadau wamekuwa wakiunganisha nguvu
kwa ajili ya kushughulikia masuala ya kuimarisha ulinzi kwa watoto wenye umri
chini ya miaka minane, afya, lishe, elimu na masuala mengine mtambuka kwa kundi
hilo muhimu katika jamii.
Alisema kuwa, pamoja na wadau wengine kutimiza vyema wajibu wao kupitia
Programu Jumuishi ya Taifa, Serikali nayo imeongeza bajeti ya lishe kwa mtoto
kwa kila halmashauri kutoka 1,000/- kwa
mwaka wa fedha 2020/21 hadi 1,239/- kwa mwaka 2021/2022.
Wataalamu wa afya ya Mama na Mtoto wanasema kuwa pamoja na udumavu,
ukondefu na uzito pungufu, suala la lishe duni ni miongoni mwa sababu za homa
za mara kwa mara kwa mtoto.
“Lishe duni ni chanzo mojawapo cha magonjwa na vifo kwa watoto wadogo; hasa
walio chini ya miaka mitano. Pia hudumaza ukuaji wa kimwili na kiakili"
alisema Dk Suleiman Muttani, Daktari Bingwa Mshauri wa magonjwa ya wanawake na
watoto hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida.
"Kama hiyo haitoshi, lishe duni pia hupunguza uwezo wa mtoto kufanya
vizuri awapo shuleni na ufanisi wa kazi katika maisha yake ya utu uzima hapo
baadae" aliongeza Dk Muttani.
Wazazi, walezi na wataalamu kutoka Mashirika, Asasi na Taasisi
zinazoshughulikia ustawi wa mtoto, wanasema njia pekee ni kuendelea kutoa elimu
kwa jamii juu ya umuhimu wa lishe bora kwa mtoto ndani ya siku 1,000 za awali ili kujenga afya
bora.
“Unaweza kushangaa tatizo kubwa la lishe duni kwa watoto lipo vijijini
kuliko mjini wakati huko ndiko vyakula vingi vya asili na vyenye virutubisho
vinapatikana. Kwa hiyo, shida ni elimu kwa jamii” Mama Amina Ali wa Kibaoni
Singida mjini alisema.
Ofisa Maendeleo ya Jamii mstaafu na Mtafiti wa masuala ya mila na desturi
za Wanyaturu, Patrick Mdachi alisema imani potofu miongoni mwa jamii; hasa
vijijini juu ya ulaji wa baadhi ya vyakula muhimu vinavyoshauriwa na wataalamu
wa afya ili kujenga mwili wa mjamzito na mtoto, ni kikwazo kingine.
“Huwezi kuamini ila jaribu kutoka nje kidogo ya mji. Kuna wajawazito na watoto hawali mayai, maini, firigisi na vyakula vingine vingi muhimu eti kwa kukatazwa na Wazee wa kiume. Hii inaturudisha nyuma sana” alieleza Mdachi na kutaka wadau kushirikiana na Viongozi wa dini, Wazee wenye uelewa na wataalamu wa afya kukemea mila hizo potofu.
Post A Comment: