Na Mwandishi Wetu
WACHIMBAJI madini wa Umoja wa Kwahemu wa Kijiji cha Yobo, Kitongoji cha
Yobo Kata ya Anet iliyopo Chamwino Dodoma wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan
awapatie eneo la kuchimba madini ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuiingizia
serikali mapato.
Ombi hilo limetolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa wachimbaji hao, Hussein
Kimolo alipokuwa akizungumza na waandishi
wa habari hii kwa niaba ya wananchi 300 waliounda umoja wa vikundi 14
vya wachimbaji.
Kimolo alisema wameamua kumuomba rais kwa kuwa ni kiongozi mkuu wa taifa
letu na ni mama anayeelewa changamoto zinazowakabili wananchi hususan wa kipato
cha chini.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa, tayari wameanza kuchimba madini kwenye eneo
lisilo na tija walilopewa na wizara ya madini.
Alisema, baada ya kuona hawanufaiki kiuchumi zaidi ya pesa wanazopata
kuishia kulipa mapato ya serikali walipeleka ombi kwa viongozi wa madini na
wakuu wa mkoa wa Dodoma waliopita kabla ya huyu wa sasa, Rosemary Senyamule ili
wapewe viwanja vitatu vyenye tija kwenye eneo linalomilikiwa na Kampuni ya Ruvu
Gemstone Mining inayomilikiwa na mzungu raia wa Ugiriki aitwaye Milcan Dimist
bila mafanikio.
Akielezea kwa undani sababu iliyowafanya wamuombe Mama Samia awepe eneo
hilo la kuchimba madini, Kimolo alisema;
“Shughuli ya uchimbaji tunaifanya baada ya kukata leseni za kuchimba madini
aina ya nikeli kwenye viwanja vitano kati ya tisa ambavyo mzungu Dimist
anavimiliki alivyovikatia leseni nane zenye ukubwa usiopungua hekta 6 kwa kila
leseni.
Aliongeza kuwa waliomba viwanja hivyo vitano na kukata leseni kufuatia
mzungu huyo tangu aliporithi viwanja hivyo kwa baba yake ambaye ni marehemu
zaidi ya miaka 33 iliyopita kushindwa kuchimba kwenye viwanja vyote isipokuwa
kimoja tu.
“Tulipobaini jinsi serikali inavyokosa mamilioni ya fedha za kodi kupitia
mzungu huyo kushindwa kuchimba kwenye viwanja hivyo, tulimuomba aliyekuwa mkuu
wa mkoa wa Dodoma wakati huo, Bilnith Mahenge atugawie viwanja vitano kutoka
anavyomiliki mzungu huyo akatushauri tuunde vikundi na kukata leseni, tukafanya
hivyo.
“Tangu tulipokata leseni hizo mwaka 2019 tumepewa viwanja viwili visivyo na
tija ambavyo miaka thelathini na tatu iliyopita kampuni ya Kolea ilichimba
madini na kuacha mashimo tupu,” alisema Kimolo.
Alivitaja viwanja hivyo kuwa ni namba PML 0382 D0M na namba PML 0381 ambapo
hadi leo hawajapewa vitatu vilivyobaki vilivyopo eneo lenye madini hivyo kupata
hasara ya kulipa mapato ya serikali bila ya kuzalisha chochote kwa upande wao.
“Kinachoshangaza ni sisi kushindwa kupewa viwanja hivyo na kuishia kwenda
kwa viongozi mara kwa mara kuwalilia wasikie kilio chetu bila mafanikio wakati
tunaishi Wilaya ya Chamwino ambayo ina makazi ya rais wetu ambapo ni rahisi
suala letu kushughulikiwa na kupata ufumbuzi,” alisema mwenyekiti huyo.
Aliongeza kuwa, hawana nia mwekezaji huyo aporwe viwanja vyote kwani
itakuwa si kumtendea haki kwa sababu serikali inawahitaji wawekezaji.
“Sisi tunamuomba mama Samia atupe viwanja vitatu vikiwemo viwili tunavyochimba visivyo na tija ili mzungu anayemiliki hekta zaidi ya 97 za ardhi yenye madini abaki na vinne licha ya kuwa na uwezo wa kuchimba katika kiwanja kimoja tangu alipoanza kuchimba madini hayo zaidi ya miaka 33 iliyopita ili tuiingizie serikali yetu mapato huku na sisi tukiinua vipato vya familia zetu kwani umoja wetu wa watu 300 unawakilisha kundi kubwa la watu,” alisema Kamolo.
Post A Comment: