Na Abby Nkungu, Singida
UKATILI wa kijinsia na unyanyasaji kwa watoto wenye umri chini ya miaka
minane umepungua kwa zaidi ya asilimia
47 katika halmashauri za Wilaya ya Singida, Ikungi na Manyoni mkoani Singida
kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka
jana.
Taarifa rasmi iliyotolewa na Mkuu wa dawati la jinsia la Jeshi la Polisi
mkoa wa Singida, Mkaguzi wa Polisi Amina
Bendera inaonesha kuwa, vitendo
hivyo vimepungua kutoka makosa 154
kuanzia Januari hadi Juni mwaka jana 2021 na kufikia makosa 81 kwa
kipindi kama hicho mwaka huu.
Katika taarifa hiyo, Mkaguzi wa Polisi Amina amefafanua kuwa halmashauri ya
Wilaya ya Singida kuanzia Januari hadi
Juni mwaka jana iliripoti matukio 100 ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji kwa watoto wa chini ya miaka
minane lakini mwaka huu kwa kipindi hicho yameripotiwa makosa 38 tu.
Alieleza kuwa katika wilaya ya Ikungi
makosa hayo yamepungua kutoka 30
mwaka jana hadi 23 mwaka huu wakati
Manyoni takwimu zinaonesha
kupungua kwa matukio hayo ya ukatili kutoka
24 hadi 20 Juni mwaka huu.
Mkuu huyo wa dawati la jinsia la Polisi mkoa wa Singida, aliyataja baadhi
ya makosa hayo kuwa ni pamoja na ubakaji, kujaribu kubaka, kulawiti, kunajisi,
ukeketaji, vipigo na kujeruhi watoto.
Alisema kuwa pamoja na usimamizi na utekelezaji wa sheria unaofanywa na
vyombo mbalimbali, juhudi kubwa za Serikali na wadau wake katika kutoa elimu
kwa jamii juu ya kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto ni
miongoni mwa sababu za kuanza kupungua
kwa vitendo hivyo.
“Kuna hii Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya
Awali ya Mtoto iliyoanza kutekelezwa Januari mwaka jana na inaendelea hadi
mwaka 2026, imesaidia sana kufikia mafaniko hayo maana kila mdau wa mtoto
anatekeleza vyema wajibu wake katika eneo la malezi, ulinzi, afya, lishe, elimu
na mengine mengi; hivyo kufanya kazi yetu kuwa rahisi” alisema Inspekta Amina
Hata hivyo, wadau wanasema kuwa pamoja na taarifa ya polisi kuonesha
mafaniko hayo ya kuanza kupungua kwa matukio ya vitendo vya ukatili na
unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto,
bado kuna haja ya kuongeza nguvu
zaidi ya elimu katika jamii ili kupinga na kutokomeza kabisa uhalifu huo.
“Sisi ndio tupo katika jamii, tunaona na kusikia mengi,
bado vitendo hivyo vipo isipokuwa sio vyote vinavyoripotiwa kwenye ofisi za
Serikali, polisi au vyombo vingine vya sheria. Wengine wanamaliza nyumbani kesi hizo kwani hufanywa na ndugu wa karibu”
alisema Magdalena Soteri mkazi wa Kindai
mjini Singida na kuungwa mkono na Ramadhani Hamisi wa eneo la Unyankhae.
“Ni elimu tu hakuna njia nyingine kama kila mtu kuanzia mzazi, mlezi na
jamii nzima atakuwa mlinzi wa mtoto na kutooneana huruma na kumaliza kindugu
kwa mtuhumiwa anayetenda makosa hayo ni dhahiri kuwa vitendo hivyo vitabaki
kuwa historia katika jamii yetu” alisisitiza Ramadhani.
Watalamu wa afya wanasema kuwa zipo athari nyingi ambazo huwakumba watoto
waliofanyiwa ukatili wa kijinsia na unyanyasaji zikiwemo za kisaikolojia,
kimwili, kiafya, na kiakili.
Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto
inasema utafiti mdogo uliofanywa na Benki ya Dunia kwenye jamii kuhusiana na
ukatili, unyanyasi na utelekezaji watoto wadogo unaofanywa na wazazi mkoani
Katavi ulionesha asilimia 18 ya wazazi wenye watoto chini ya miaka mitatu kuwapiga
vibao watoto wao.
Nazo tafiti za awali za mradi wa malezi uliofanywa na Shirika la EGPAF
wilayani Nzega, Igunga na Tabora Manispaa uliripoti kuwa asilimia 53 ya wazazi
wa watoto wenye umri wa miaka 0 - 2 wanaamini kuwa watoto lazima waadabishwe
kwa kuchapwa.
Hata hivyo, hakuna takwimu zinazoonesha picha halisi ya ukatili, unyanyasaji na utelekezaji watoto Kitaifa.
Post A Comment: