Dawa zinazotumiwa na wajawazito wanaoishi na virusi vya Ukimwi (VVU) kukinga maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto zimeonyesha kujenga usugu kwa kiwango kikubwa kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mikoa 19 Tanzania.
Matokeo ya utafiti huo uliofanywa katika mikoa 19 umeonyesha dawa hizo zimejenga usugu kwa asilimia 27.5 kwa kinamama waliogundulika na maambukizi wakati wa ujauzito ambao hawajaanza kutumia dawa na asilimia 79.2 kwa wale ambao tayari wapo kwenye matumizi ya dawa za kufubaza makali yaani ARV.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Septemba 22, 2022 wakati Kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa Marekani (CDC) kupitia Menejimenti na Maendeleo ya Afya (MDH) kutoa matokeo ya tafiti tatu zilizofanywa nchini kuangalia udhibiti wa mlipuko, kinga na tiba ya vvu wakati wa ujauzito na kunyonyesha.
Kiongozi wa utafiti huo uliolenga kutathmini kiwango cha maambukizi, mwelekeo na vihatarishi vya usugu wa dawa kabla ya matibabu (PDR) na baada ya matibabu (ADR) Dk Boniphace Jullu amesema matokeo hayo yanatakiwa kuwaamsha watunga sera kuangalia nini wanafanya ili kufikia malengo ya millennia SDGs.
“Tulisajili wanawake wajawazito 459 ambao hawakuwa katika matumizi ya dawa na 543 walio na uzoefu wa matumizi ya dawa kwa pamoja kutoka kliniki 52 zilizochaguliwa bila mpangilio maalum katika mikoa 19 kuanzia Aprili hadi Septemba 2019.
“Matokeo yetu yalionyesha kuwa maambukizi ya PDR na ADR yalikuwa juu kwa asilimia 27.5 na asilimia 79.2 kwa mtiririko huo. Kwa ujumla, wengi wa washiriki wasiojua hali zao waliambukizwa na virusi vya ukimwi sugu. Amesema
Ofisa Mtendaji Mkuu wa MDH, Dk David Sando amesema licha ya kuwepo kwa huduma nyingi za kliniki zinazosaidia nchini Tanzania kwa asilimia 93 bado maambukizi ya vvu kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ni makubwa kwa asilimia 11.
“Usugu wa dawa za vvu ni tishio moja zaidi kwa ufanisi wa ARV. Taarifa kuhusu usugu wa dawa zinapatikana lakini hazijumuishi wanawake wajawazito wanaoishi na vvu.
“Taarifa hii ni muhimu katika kufahamisha watunga sera ili kuongeza uboreshaji wa huduma za matunzo kwa kundi hili,” amesema Dk Sando.
Post A Comment: