Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Kigoma, Bw. Ntime Mwalyambi, akifungua mafunzo kuhusu kanuni ya mashirikiano kati ya TBS na Maafisa Afya na Biashara wa Halmashauri za mkoa wa Kigoma mapema leo, Bw. Mwalyambi amewataka washiriki wote kuzingatia mafunzo hayo ili kuweza kutumia utaalamu watakaoupata na kuwahudumia wananchi kwa weledi.Mafunzo haya yamefanyika pia katika Halmashauri za mikoa ya Mtwara, Tanga, Pwani na Mwanza na yanatarajiwa kufanyika katika Halmashauri zote nchini.

*********** NA MWANDISHI WETU ************ 

SHIRIKA la viwango nchini (TBS) limesema kuwa mafunzo yanayoendelea  kutolewa na shirika hilo kwa maafisa afya na maafisa biashara wa halmashauri kwenye mikoa mbalimbali nchini yataimarisha usimamizi wa sheria na taratibu za kiutendaji zinazopaswa kufuatwa na wazalishaji na wauzaji wa bidhaa za chakula na vipodozi nchini na kuondoa migongano inayoweza kujitokeza.

Meneja utafiti na mafunzo kutoka TBS, Hamisi Sudi akizungumza wakati wa mafunzo kwa watendaji hao alisema kuwa mafunzo hayo yanakuja ikiwa sehemu ya mkataba wa ushirikiano baina ya Wizara ya Biashara na Wizara ya Tawala za mikoa na serikali za mitaa ili usimamizi wa sheria na kanuni zielewe bayana na kuondoa migongano kweye utekelezaji wake.

Alisema kuwa katika muundo wa sasa ambapo baadhi ya shughuli zilizokuwa zikifanywa na Mamlaka ya chakula na dawa  (TFDA) ambayo kwa sasa inafahamika kama Mamlaka ya udhibiti wa dawa na vifaa tiba (TMDA) zimehamishiwa TBS hivyo kuongeza majukumu ya kiutendaji hivyo mafunzo hayo yanalenga kuwatumia maafisa wa halmashauri kusaidia kusimamia utekelezaji wa majukumu hayo.

Sudi alisema kuwa Sheria namba nane ya fedha ya mwaka 2019 ya kuimarisha usalama na udhibiti wa bidhaa za vyakula na vipodozi pamoja na usajili wa bidhaa hizo, majengo ambayo yanatumiwa kuzalisha au kuuza jukumu ambalo shirika hilo halina idadi ya kutosha ya kusimamia na hivyo kutumia maafisa biashara na maafisa afya katika halmashauri kusimamia utekelezaji wa majukumu hayo.

Ofisa Ukaguzi kutoka TBS makao makuu Baraka Mbajije ambaye ni mratibu wa mafunzo hayo alisema kuwa jambo kubwa ambalo wanalifanya ni kufundisha kanuni za usimamizi kwa watendaji wa halmashauri wanaosimamia jukumu la usimamizi wa usalama wa chakula na vipodozi na nyongeza ya majukumu baada ya baadhi ya majukumu ya TFDA kuhamishiwa TBS.

Kwa upande wake Afisa biashara kutoka sekretariet ya mkoa Kigoma,Omari Ndimuligo alisema kuwa mafunzo hayo kwao ni muhimu katika kujua sheria,taratibu na miongozo katika kusimamia jukumu walilopewa la kusimamia udhibiti wa usalama wa vyakula na vipodozi.

Ndimuligo alisema kuwa ni jambo jema kujua vizuri sheria hiyo ili isitokee migongano na kuonekana wanawaonea wafanyabiashara hasa suala la kuteketeza bidhaa vya vyakula na vipodozi ambazo hazina viwango, zilizopigwa marufuku na ambazo ni hatari kwa maisha ya binadamu.

Share To:

Adery Masta

Post A Comment: