Na. Joachim Nyambo,Katavi
Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara – TANAPA, Herman Batiho amewataka wahitimu wa Mafunzo ya Uongozi na Kwata kwa Askari Waandamizi kuisaidia Mahakama kujenga Ushahidi usio na mashaka kwa kesi zote zinazohusiana na masuala ya Wanyamapori na Misitu.
Ameyasema hayo wakati alipokuwa akihitimisha mafunzo hayo Mlele - Mkoani Katavi ambapo alisema,ni matumaini mafunzo waliyoyapata yamewajengea uzalendo,uadilifu,kujiamini na weledi katika kutimiza majukumu yao ili mbinu mbalimbali walizipata ziweze kuwasaidia katika kukabiliana na changamoto za migogoro ya uvamizi wa Wanyamapori katika makazi ya watu.
“Tumewafundisha ramani ili mnapokwenda kuwasimamia wafuasi, muwaelekeze wanapokamata majangili wasaidiane na Kitengo chetu cha Uchunguzi kuchora ramani eneo la tukio ili kujenga Ushahidi usio na mashaka, maana takwa la Mahakama kwa kesi zote zinazohusu nyara za Serikali hususani zinazohusu Maliasili sharti yawe na ramani ya maeneo wanapokamatwa Watuhumiwa”, alibainisha Kamishna Batiho.
“Mmefundishwa kusimamia na kuongoza doria halikadhalika, mbinu sahihi za ukamataji ili kuepuka kadhia na madhara mengine yanayoweza kujitokeza kwa yule anayekatwa na hata sisi wenyewe tunaokamata. Hivyo mkayazingatie yale mliyofundishwa na kufuata sheria za ukamataji ili kuondoa malalamiko yasiyo ya lazima”, alisisitiza Kamishna Batiho.
“Sambamba na hayo nisisitize mambo makuu mawili ya msingi sana, jambo la kwanza kasimamieni nidhamu kwa askari wetu halikadhali vitendea kazi vitumike vizuri nikimaanisha magari, silaha na nyumba tunazoishi” aliongeza Kamishna Batiho.
Naye Mkuu wa Mafunzo hayo Luteni Kanali Matei Msechu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWT) alisema, “licha ya muda wa Mafunzo kuwa mfupi kulingana na masomo yaliyofundishwa, wahitimu hao wanafahamu mambo mengi kuhusiana na Jeshi (Soldierly skills and qualities) hivyo watumike kama kiungo kati ya Maafisa na Askari katika Taasisi”.
Aidha Luteni Kanali Msechu aliongeza kuwa sehemu kubwa ya Mafunzo haya ilikuwa ni vipindi vya nje (practical) ili kuwajengea uwezo mkubwa katika uongozi na utendaji kazi kwa kutumia mfumo wa kijeshi ambao Taasisi zote nne zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii zimeafiki kuufuata kwani umeonekana kuwa tija katika shughuli za Kiuhifadhi.
Post A Comment: