Katibu Mkuu wa JOWUTA Selemani Msuya (kulia) akitoa maelezo kwa Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi nchini, Pendo Berege ambaye ametembelea ofisi za makao makuu ya JOWUTA yaliyopo Chang'ombe Madukani wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
MSAJILI wa Vyama vya Wafanyakazi nchini Pendo Berege, amekitaka Chama cha
Wafanyakazi wa Vyombo vya Tanzania (JOWUTA), kuongeza kasi ya usajili wa
wanachama kama Sheria na Katiba ya inavyotaka.
Msajili Berege ametoa maelekezo hayo leo Agosti 31/2022 baada ya kutembelea
ofisi za makao makuu ya JOWUTA yaliyopo Chang'ombe Madukani wilayani Temeke
jijini Dar es Salaam.
Amesema taarifa alizopatiwa na uongozi wa JOWUTA ni nzuri ila ni vema
juhudi za kupata wanachama wapya zikaongezeka ili chama hicho kiwe cha mfano
nchini.
"Nipo kwenye ziara ya kukagua uhai wa vyama, kusema kweli nawapongeza
kwa kazi mnayofanya, pamoja na changamoto mlizoanisha endeleeni kusajili
wanachama wapya kwenye vyombo vya habari.
Pia endeleeni kutoa elimu ya umuhimu wa kujiunga na vyama vya wafanyakazi
kwani ni daraja baina ya waajiri na wafanyakazi, hivyo waandishi wa habari
waone umuhimu wa kujiunga na JOWUTA," amesema.
Msajili ameshauri JOWUTA kushirikiana na taasisi nyingine zinazojihusisha
na vyombo vya habari ili kujadili na kutoka na maamuzi kuhusu sekta hiyo.
Berege amewataka waandishi wa habari kutumia JOWUTA kama jukwaa sahihi
kwenye kutatua changamoto zinazowakabili katika tasnia hiyo.
"Pia nitumie nafasi hii kuwashauri waandishi wa habari kutembelea
ofisi yao ili waweze kupata elimu na taarifa,"amesema.
Katibu Mkuu wa JOWUTA, Selemani Msuya alimuahidi Msajili Berege kuwa
wamejipanga kuwafikia waandishi wa habari katika mikoa yote kwa siku za
karibuni.
Msuya amemuambia Msajili Berege kuwa Kwa takwimu za Serikali Tanzania kuna
zaidi ya vyombo vya habari 1,000 ambavyo vina wafanyakazi zaidi 5,000 hivyo
iwapo watajiunga na JOWUTA chama hicho kitakuwa na nguvu ya kusimamia maslahi
yao.
"Tupo kwenye mkakati wa kuwafikia waandishi kote nchini, kuwapatia
mafunzo na elimu ya umuhimu wa kujiunga na JOWUTA tunaamini
tutafanikiwa,"amesema.
Katibu huyo amesema kwa sasa JOWUTA Ina wanachama zaidi ya 250 kwenye mikoa
zaidi ya 10 na mkakati wao ni kuwafikia waandishi wote kwa siku za karibuni.
Naibu Katibu Mkuu wa JOWUTA, Said Mmanga amemuambia Msajili Berege kuwa
hapa ilipofikia JOWUTA ni hatua kubwa na watahakikisha hawarudi nyuma.
Mmanga amesema matarajio yake ni kuona miaka michache ijayo JOWUTA inagusa
jamii ya waandishi kwa asilimia kubwa zaidi.
Post A Comment: