Na,Jusline Marco;Arusha


Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Misseile Albano Musa,ameipongeza halmashauri ya Arusha kwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa shule mpya ya sekondari Kiutu kwa viwango ambavyo ubora wa mradi huo unaonekana hata kwa macho licha ya kwamba mradi huo bado haujakamilika.

Misseile ametoa pongezi hizo wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya  utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa shule mpya ya sekondari Kiutu, iliyopo halmashauri ya Arusha, mradi unaotekelezwa na serikali kupitia program ya kuboresha elimu ya sekondari nchini (SEQUIP).

"Ninawapongeza wataalamu wa halmashauri ya Arusha, inaonesha namna gani mnafanyakazi kama timu, endeleeni kufanya hivyo ili kufikia malengo ya serikali ya kuwahudumia wananchi". Amesisitiza Katibu Tawala huyo.


Aidha amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, kuhakikisha mradi huo  unakamilika kwa wakati ili wanafunzi wa kidato cha kwanza wapangiwe shule hiyo na kuanza masomo ifikapo Januari 2023.

Naye Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, amemshukuru Katibu Tawala huyo kwa kutembelea mradi huo na halmashauri yake kwa ujumla ambapo ameahidi kutekeleza maagizo, yote aliyoyatoa lengo likiwa ni kuhakikisha wanafunzi wa kidato cha kwanza wanapangiwa na kuanza masomo mapema mwezi Januari 2023.

Awali akisoma Taarifa ya mradi huo kwa niaba ya msimamizi wa mardi huo, Makamu mkuu wa shule ya sekondari Kiutu Mwl. Upendo Mollel amesema kuwa mpaka sasa mradi umefikia asilimia 65 ya utekelezaji wake na makadirio ya gharama za ukamilishaji wa mradi huo ni takribani shilingi milioni 250 fedha ambazo zikipatikana mradi utakamilika mpaka mwisho.


Kwa upande wake Afisa Elimu sekondari halmashauri ya arusha Mwl. Menard Lupenza amesema kuwa Serikali kupitia program ya SEQUIP ilitoa kiasi cha shilingi milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari Kiutu, ujenzi unaojumuisha jengo la ghorofa mbili lenye kubeba vyumba 8 vya madarasa, maktaba, maabara za masomo ya TEHAMA na  vyoo vya wanafunzi, jengo la Utawala na Maabara za masomo ya Kemia, Fizikia na Baiolojia.

Share To:

JUSLINE

Post A Comment: