Kassim Nyaki, Ngorongoro.


Mifugo 5,219 ya wafugaji wanaoishi eneo la Hifadhi ya Ngorongoro hadi kufikia tarehe 1 Septemba, 2022 imehamishiwa katika Kijiji cha Msomera Handeni Mkoani Tanga tangu zoezi la kuwahamisha wananchi walio tayari kuhama kwa hiari kutoka Hifadhi ya Ngorongoro.

 

Taarifa hiyo imetolewa leo tarehe 1 Septemba, 2022 wakati wa kuaga kundi la 7 lenye kaya 25 zenye watu 159 waliondoka Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera kwa ajili ya kupisha shughuli za Uhifadhi katika hifadhi hiyo.

 

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela ameeleza kuwa tangu kuanza kwa zoezi la kuhamisha wakazi waliotayari kuhamia Msomera tarehe 16 Juni, 2022 hadi kufikia Septemba mosi 2022 jumla ya Kaya 158 zenye watu 794 na mifugo 5,219 zimehamia katika Kijiji cha Msomera Wilayani Handeni Mkoani Tanga.

 

“Zoezi hili tulianza tarehe 16 Juni, 2022, hamasa imekuwa kubwa kuliko tulivyotarajia, katika awamu zote leo kundi hili la 7 ndio lina kundi kubwa la mifugo ipatayo 2,109. Hii ni ishara njema katika kupunguza muingiliano wa Wanyamapori na Mifugo ndani ya Hifadhi” aliongeza Mongela.

 

Naibu Kamishna wa Uhifadhi NCAA Dkt. Christopher Timbuka amebainisha kuwa idadi ya wananchi wanaojitokeza kujiandikisha na kuhama kwa hiari imeendelea kuongezeka kutokana na hamasa na elimu iliyotolewa kwa wananchi hasa baada ya Serikali kujenga miundombinu ya huduma za kijamii kama shule, hospitali, huduma ya maji, majosho, Malambo, barabara, nyumba za kuishi, mashamba, nishati ya umeme pamoja na mawasiliano.

 

Dkt. Timbuka ameongeza kuwa zoezi la kuhamisha wananchi hao linazingatia misingi na taratibu zote za haki za binadamu pamoja na muongozo wa uhamishaji wa wakazi ulioandaliwa na Serikali.

 

Saruni Mapekuo kutoka Kijiji cha Kapenjiro ambaye ni mmoja wa wananchi wanaohama kwa hiari ameeleza kuwa;

 

“Tunashukuru kwa fursa hii tuliyopewa na Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kutupa fursa ya kuhama Ngorongoro kwenda Msomera.


 Hii imetusaidia kufunguka kiakili kwa kuchangamana na wananchi wengi, naamini baada ya mwaka mmoja nitakuwa nimejiendeleza kibiashara, kilimo na kufuga Ng’ombe wa kisasa na bora na kuachana na kufuga mifugo mingi ambayo haina tija”.


Zoezi la uhamasishaji na uandikishaji wa Wananchi kuhama kwa hiari linaendelea, ambapo hadi kufikia tarehe 31 Agosti, 2022 jumla ya kaya 1,019 zenye jumla ya watu 5,667 na Mifugo 13,927 zimejiandikisha kuhama kwa hiari katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.








Share To:

Post A Comment: