Na Imma Msumba ; Mbulu
Katika kuhakikisha vipaji vya riadha vinakuzwa na kuendelezwa katika mkoa wa Manyara na kupata medali mbalimbali, Halmashauri ya mji wa Mbulu imejipanga kuanzisha timu ya riadha (Mbulu Town Council Athletic Club).
Mpango huo wa Miaka Mitano ambao utekelezaji wake unaandaliwa, umelenga medali zote ambazo zinatafutwa Tanzania ziwe zinatokea Mbulu kupitia wakimbiaji watakaokuwa wameandaliwa vyema.
Kwa mujibu wa Afisa Michezo katika Halmashauri hiyo Benson Maneno,Klabu hiyo ya riadha pekee itakuwa chini ya Umiliki wa Halmashauri ya mji wa Mbulu.
Benson anaeleza "Hii klabu itakuwa inashiriki mashindano yote kitaifa na kimataifa,tutashirikiana na wadau wengine na tutaajiri kocha mwenye kiwango cha kimataifa kwa msaada wa chama cha Riadha Tanzania".
Wilaya ya Mbulu ina historia katika mchezo wa riadha kupitia wachezaji mbalimbali akiwemo John Stephen Akhwari ambaye anakumbukwa kwa kushiriki katika michezo ya Olimpiki ya mwaka 1968 nchini Mexico.
Mwanariadha huyo licha ya kumaliza akiwa wa Mwisho alinukuliwa akisema ''Taifa langu halikunituma Mexico kuanza mbio bali kumaliza, ni kutaka kwangu na uzalendo nilionao katika maisha yangu kama mwanariadha ndio ulionifanya kumaliza mbio hizo".
Post A Comment: