Na John Walter-Manyara
Mkuu wa mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere amesema katika maadhimisho ya siku Fimbo nyeupe yatakayofanyika kuanzia oktoba 19 mwaka huu yataambatana na maonesho ya kibiashara kwa lengo la kuonesha fursa mbalimbali zinazopatikana ndani ya mkoa wa huo.
Makongoro amezungumza hayo leo Septemba 23,2022 mbele ya waandishi wa habari katika ofisi yake iliyopo Mjini Babati na kuwasihi Wanamanyara kutumia fursa hiyo vizuri kwa kuleta biashara zao siku ya maonesho.
Maonesho hayo yanayoongozwa na kuratibiwa na ofisi ya mkuu wa mkoa kupitia Chemba ya wafanyabiashara, wenye viwanda na wakulima (TCCIA) mkoa wa Manyara, yanayokwenda kwa jina la Tanzanite Trade Fair Exhibition yanatarajiwa kuonesha fursa mbalimbali zinazopatikana ndani ya mkoani hapa zikiwemo kilimo, Madini ya iana mbalimbali, shughuli za utalii pamoja na biashara aina tofauti.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya mkuu wa mkoa, maonesho hayo ya kibiashara yanatarajiwa kuanza Oktoba 19,2022 hadi Oktoba 23, 2022 huku Wanamanyara wakiombwa kujiandaa kupokea wageni mbalimbali kutoka maeneo tofauti ya nchi ya Tanzania watakaohudhuria katika maonesho hayo yatakayoambatana na ya siku ya Fimbo nyeupe ambayo kitaifa mwaka huu yatafanyika kitaifa mkoani Manyara huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa waziri mkuu Kassim Majaliwa.
Aidha mkuu wa mkoa amewaalika wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kuja wekeza katika viwanda vya nyama kwa kuwa kuna mifugo ya kutosha inayopatikana na mpaka sasa uongozi wa mkoa unaendelea na mikakati madhubuti ya kuhakikisha mifugo inaongezeka kwa wingi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya Mati Super Brand David Mulokozi ambao ni wadhamini wakuu katika maonesho hayo, amesema kwa upande wao ni fursa nzuri kwani itawawezesha kukutana na wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali na kutanua wigo wa biashara zao.
Kauli mbiu ya maonesho ya hayo ya kibiashara Tanzanite Trade Fair Exhibition, inasema “Manyara ipo tayari na imefunguka kibiashara”.
Fimbo nyeupe ni maadhimisho yanayowalenga watu wenye changamoto ya kushindwa kuona ili kuwaleta karibu na wanajamii na kuwa sehemu ya faraja kwao kwa ishara hiyo ya kuoneshwa thamani, si hivyo tu bali pia watanzania hawa wenye matatizo ya kushindwa kuona hupata nafasi ya kuonesha vipawa vyao na kupata nyenzo wezeshi zitakazowasaidia kujiendeleza kiuchumi.
Post A Comment: