MBUNGE wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha mchakato wa ujenzi wa lami Barabara ya kilomita 223 kutokea Mto Rumemo Ifakara hadi Madeke ilipo boda ya Mkoa wa Morogoro na Njombe.


Kunambi amesema hayo kwenye mkutano wake wa hadhara katika Kata za Masagati na Utengule ambapo ameeleza kuwa kwa kuanzia tayari maelekezo yameshaanza ya kuanza kwa awamu ya kwanza ya ujenzi huo ambapo utaanza na kilomita 50 kuanzia Ifakara hadi Mbingu kisha awamu ya pili yenye kilomita 37 kuanzia Mbingu hadi Chita itafuata.


Amesema kilio cha kuwepo kwa Barabara ya Lami itakayounganisha Mkoa wa Morogoro na Njombe kimekua ni kilio cha wananchi wa Mlimba kwa muda mrefu lakini sasa kinaenda kuisha baada ya Rais Samia kuelekeza kuanza kwa ujenzi huo ambao utazidi kufungua na kuchochea fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Mlimba.


" Kipekee nimshukuru Sana Rais Samia ndani ya muda mfupi baada ya kuingia madarakani ameelekeza kuanza kwa ujenzi wa Barabara kiwango cha Lami kutokea Ifakara hadi Madeke ilipo boda ya Morogoro-Njombe, kwa kuanzia tutaanza na km 50 kutokea Ifakara hadi Mbingu kisha km 37 zitafuata kutokea Mbingu hadi Chita.


Kama hiyo haitoshi kupitia mahusiano mazuri aliyoyaweka Rais Samia tumepata ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) ambapo wao watawezesha ujenzi wa km 93 kiwango cha lami kutokea Kihansi Mlimba hadi Madeke Njombe, hapa Uchumi wetu wananchi wa Mlimba utakua umefunguka kwa kiwango kikubwa,"Amesema Kunambi.


Kunambi pia amemshukuru Rais Samia kwa kulipatia Jimbo la Mlimba fedha za Uviko-19 kiasi cha Sh Bilioni 1.7 fedha ambazo zimetumika kuwezesha miradi ya sekta mbalimbali ikiwemo Elimu na Afya.


" Kupitia fedha za Uviko-19 Rais Samia ameligusa Jimbo letu la Mlimba kwa kiasi kikubwa, tumefanikiwa kupata Sh Bilioni 1.77 ambazo tumejenga Madarasa 80 sawa na Sh Bilioni 1.6, Bweni la watoto wenye mahitaji Maalum lenye thamani ya Sh Milioni 80 katika Kata ya Igima na nyumba ya watumishi wa afya iliyogharimu Sh Milioni 90.


Kwa kutambua changamoto ya Mawasiliano iliyopo kwenye baadhi ya maeneo hapa Mlimba nimejenga hoja na Serikali imesikia kilio chetu ambapo kwenye mwaka huu wa fedha kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari tumepata minara mitano ambayo itafungwa kwenye Kata za Mofu, Udagaji, Uchindile, Masagati na Ching'anda. Yote haya ni katika kuchochea maendeleo kwenu nyinyi Wananchi wetu," Amesema Kunambi.


Katika ziara hiyo pia Kunambi alieleza kuwa kuanzia Januari wanatarajia kuanza ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Masagati  ambapo kwa kuanzia yeye kama Mbunge atachangia Sh Milioni Tano lakini pia akiwezesha kupatikana kwa Sh Milioni 14 zitakazowezesha kuanza kwa ujenzi wa Madarasa katika Shule ya Msingi Ipinde.







Share To:

Post A Comment: