Na Dotto Mwaibale, Ikungi
HALMASHAURI yaWilaya ya Ikungi mkoani Singida imeanza mkakati mpya wa kutafuta vyanzo vipya vya mapato wenye
lengo la kuongeza mapato baada ya chanzo chao kikubwa cha mazao ya biashara
kuporomoka kutokana na uhaba wa mvua.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally
Mwanga wakati akifungua kikao cha kawaida cha baraza la madiwani ambacho ni cha
mwisho wa mwaka kilichoketi leo wilayani humo.
"Tumekwisha ingia mwaka mpya wa fedha na kama mnavyojua kuwa jiografia
ya halmashauri yetu mvua zikinyesha chini ya kiwango zinasababisha mazao
kupungua kama vile alizeti, mpunga, dengu na mazao mengine" alisema
Mwanga.
Alisema baada ya kutokea hali hiyo walishauriana kuangalia vyanzo vya
mapato vya uhakika ambavyo vitaisaidia
halmashauri hiyo kukusanya mapato na kuwa mpango wa kwanza utaanzia Stendi ya
mabasi ya Kata ya Mungaa ambapo kama watasimamia vizuri ukusanyaji wa mapato
baada ya magari kuingia katika stendi hiyo
kwa mwezi watapata Sh. 16 Milioni
na zaidi ya fedha hiyo.
Mwanga alisema maeneo mengine watakayo yaangalia ni stendi ya mabasi ya
Isuna, Ikungi, Ihanja, Sepuka na maeneo mengine yanayofananana na hayo na kufungua minada Kijiji cha Choda na Chungu jambo
ambalo litasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza mapato ya halmashauri hiyo.
Alisema kuacha magari yakipita bila ya kuweka utaratibu wa kuingia stendi
zitakazoanzishwa itakuwa ni hasara kwa halmashauri hiyo ambapo alitumia nafasi
hiyo kuziomba kila kata yanapopita magari hayo ni lazima watengeneze stendi
hizo.
Mwanga alitaja vyanzo vingine wanavyotarajia kuvianzisha kuwa ni pamoja na
kufungua minada maeneo mengine ndani ya halmashauri hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi
alisema anakubaliana na mkakati wa
madiwani hao wa kuanzisha mpango huo kabambe wa kuwa na vyanzo vya
mapato na akasisitiza kuwa wakipata maeneo ya kuweka stendi hizo halmashauri
itasaidia kupeleka katapila la kutengeneza maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kujenga vyoo.
Halikadharika Kijazi alisema mwaka wa fedha uliopita wa 2021/ 2022 halmashauri hiyo imeweza kufikia asilimia 102 ya kukusanya mapato lakini akasisitiza kuwa itakuwa haina maana kukusanya mapato kwa wingi na matumizi yakawa ni makubwa na kueleza kuwa wanakwenda kuondoa posho zisizo za lazima na fedha hizo watazielekeza kwenye miradi ya kupata fedha zaidi.
Alisema mafanikio ya kufikia asilimia hiyo yametokana na ushirikiano mzuri baina ya madiwani na watumishi wa kada nyingine wa halmashauri hiyo na lengo likiwa ni kuiletea maendeleo.
Katika hatua nyingine Kijazi aliliomba baraza hilo la madiwani kupitisha Sh.100 Milioni kwa ajili ya kuifunga stendi ya mabasi ya Ikungi akitolea mfano stendi ya Manyoni ambayo kila siku wanakusanya Sh.Milioni 3.5 mabasi yanapopita hivyo ikifunguliwa wataweza kupata Sh. Milioni 3 hadi 4.
Aidha Kijazi alisema watendaji wote watakao onekana wakilegalega katika suala zima za ukusanyaji wa mapato kwenye maeneo yao watawaondoa.
Diwani wa Kata ya Unyahati, Abel Suri alisema uanzishaji wa vyanzo hivyo
vya mapato ni jambo la lazima ambapo aliomba ufanisi na nguvu katika ukusanyaji
wa mapato hayo iongezeke hasa kwa watendaji wa kata.
"Tunawaomba watendaji wote wa
kata wawajibike na kuongeza bidii ya kukusanya mapato kwani hiyo ni moja ya
kazi yao kubwa na hata katika mkataba wao wa kazi jukukumu hilo lipo" alisema Suri.
Suri alisema moja ya kipimo cha utendaji kazi wa maafisa hao ni ukusanyaji
wa mapato na si vinginevyo.
Katika kikao hicho ajenda kubwa ilikuwa kila kata kutoa taarifa ya
ukusanyaji wa mapato ambapo kata nne zilizofanya vizuri zilitoa taarifa halikadharika
kata nne ambazo zilizofanya vibaya nazo zilitoa taarifa na sababu
zilizojitokeza mpaka zikafanya vibaya na hatua zitakazofanyika ili kuongeza
mapato.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ikungi Mika Likakapa ambaye alikuwa mgeni mualikwa katika kikao hicho alisema madiwani hao wanapaswa kuzingatia vyanzo vya mapato vikubwa na si vile vidogo vidogo ambavyo vinaweza kuwaletea wananchi usumbufu na kuleta changamoto.
Kesho baraza hilo la madiwani litaketi tena ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.
Post A Comment: