Na Asteria Muhozya, Igunga

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amemwagiza Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Tabora kuanza mchakato wa kuanzisha Kituo cha Ununuzi wa Madini katika Wilaya ya Igunga ili kurahisisha biashara ya Madini  katika Wilaya hiyo  inayoongoza kwa uzalishaji wa madini mkoani Tabora.

Kwa mujibu wa taarifa ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Tabora inabainisha kuwa, Wilaya ya Igunga ndiyo inayoongoza katika uzalishaji wa dhahabu mkoani humo ikifuatiwa na wilaya ya Nzega, Sikonge na Kaliua.

Aidha, taarifa hiyo inaonesha kuwa,  mzunguko wa fedha katika soko la madini Tabora umefikia shilingi bilioni 48 zinazotokana na biashara ya kuuza na kununua dhahabu  inayofanywa na  wafanyabiashara 17 waliopo katika soko kuu la mkoa ambao wanategemea dhahabu inayozalishwa na wachimbaji wadogo  kutoka wilaya za mkoa huo.

Kufuatia mafanikio hayo na kutokana na mwenendo mzuri wa makusanyo ya maduhuli ya Serikali, Dkt. Kiruswa  ametoa siku 90 kwa Afisa Madini Mkazi kuhakiki na  kuwasilisha wizarani taarifa za walio hodhi leseni zao bila kuziendeleza kwa kipindi kirefu ili maeneo hayo wapatiwe watu wengine wenye nia ya kuwekeza.

Vilevile, katika jitihada za kuendelea kuwawekea wachimbaji mazingira mazuri ya  kufanya shughuli zao  kwa tija, Dkt. Kiruswa amezitaka Taasisi za Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania ( GST) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kufika mkoani humo kuangalia eneo ambalo  linaweza kutumiwa kwa uwekezaji wa mtambo wa kuchenjua  marudio ya dhahabu suala ambalo wachimbaji wameiomba Serikali kuliangalia.

Ameongeza kwamba, wizara imeweka mpango kabambe wa kuwasaidia wachimbaji wadogo kuhakikisha wanachimba bila kubahatisha kwa kuiwezesha STAMICO kuja na mkakati wa kununua mtambo wa uchorongaji kwa ajili shughuli za wachimbaji wadogo.

" Tunataka kuona wachimbaji wadogo wanachimba kwa tija na wanakua kutoka kwenye uchimbaji mdogo," amesema Dkt. Kiruswa.

Kadhalika, ameendelea kusititiza suala la wachimbaji  wadogo kujiunga katika vikundi ili kupata huduma kwa urahisi.

Katika hatua nyingine,    Dkt. Kiruswa amewapongeza wachimbaji wadogo Daudi Mwita mmiliki wa kampuni ya Kasala Gold Limited na Meneja Mkuu wa Kampuni ya TAUR Tanzania Limited kutokana na uwekezaji mkubwa walioufanya ikiwemo kufanya uchimbaji wa kisasa, uwekezaji kwenye jamii na kutoa nafasi kwa wachimbaji wengine  kukua na kujipatia vipato.

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Tabora Mayigi Makolobela amewataka wachimbaji kutunza takwimu zao za biashara  ikiwemo taarifa za uzalishaji na kufuata mfumo rasmi wa kibiashara wa Serikali ili iwe rahisi kukopeshwa na taasisi za fedha.

Ameongeza kuwa, Ofisi yake itaendelea kutoa elimu kuhusu kuingia makubaliano ya kibiashara, uchimbaji  salama na wenye tija, pamoja na mambo mengine yanayohusu sekta hiyo.

Ameendelea kuwasisitiza wachimbaji kupima madini na kaboni zao kwa kina kabla ya kuchenjua ili kuepusha malalamiko ya kuibiwa katika viwanda vya kuchenjua dhahabu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Igunga  Sauda Mtondoo amezipongeza kampuni za TAUR Tanzania Limited  na  Kasala Gold Limited  kutokana na uwekezaji uliofanywa kwenye wilaya hiyo ikiwemo  huduma za kijamii ambazo kampuni hizo zimechangia kwa jamii.

Ziara ya Naibu Waziri ililenga kuangalia maendeleo ya shughuli za wachimbaji mkoa wa Tabora, kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili wachimbaji ikiwemo mwenendo wa Sekta ya Madini mkoani humo.

Share To:

Post A Comment: